Ruto: Ndugu zetu Watanzania, tunaomba msamaha kama tumewakosea
RAIS William Ruto ameomba msamaha vijana na mataifa jirani Tanzania na Uganda, katika hatua inayofasiriwa imetokana na malumbano makubwa ambayo yamedumu mitandaoni kwa wiki mbili sasa kufuatia kisa kilichoanza na kufurushwa kwa kinara wa PLP Martha Karua.
Bi Karua, pamoja na wanaharakati wengine wakijumuisha Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga walizuiwa kuingia nchini Tanzania kuhudhuria kusikizwa kwa kesi ya uhaini ya Kiongozi wa Chadema Tundu Lissu.
Serikali ya Tanzania haikutoa taarifa rasmi kuhusu sababu za kuzuiwa kwa wanaharakati hao.
Lakini ni tukio la kuzuiliwa, kuteswa, kusafirishwa na kutupwa Ukunda, Kwale kwa mwanaharakati maarufu Boniface Mwangi, pamoja na ripoti za kubakwa kwa mwanaharakati wa Uganda Agather Atuhaire aliyekuwa ameandamana naye ndio kulizua hasira kubwa miongoni mwa watumiaji mitandao — kisa kilichosababisha Serikali ya Amerika vile vile kuitaka Tanzania kuchunguza madai hayo.
Jumatano, Mei 28, 2025 wakati wa hotuba yake kwa taifa katika hafla ya Maombi ya Kitaifa ambayo huleta pamoja viongozi wa serikali, Rais Ruto alisema ikiwa kuna jinsi viongozi wamewaendea visivyo vijana wa Gen Z, basi anaomba radhi.
“Tunataka kutembea hii safari pamoja, kujenga mahusiano kwa misingi ya kuheshimiana na kuelewana.”
“Kwa majirani zetu Tanzania, ikiwa tumewakosea kwa vyovyote vile, tunaomba radhi kwa mioyo yetu yote. Tafadhali tusameheni. Kwa ndugu na dada zetu Uganda, ikiwa kuna vile tumewaendea visivyo, tunaomba msamaha wenu.”