Ruto, Raila wachafua Msambweni
MOHAMED AHMED NA FADHILI FREDRICK
GHASIA zilizoshuhudiwa mwaka 2019 kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra jijini Nairobi kati ya wafuasi wa Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, zilijirudia Jumanne katika kinyang’anyiro cha Msambweni, Kaunti ya Kwale.
Wanasiasa wa mirengo ya wawili hao kutoka nje ya Kaunti ya Kwale walidaiwa kuchochea ghasia hizo pamoja na kuhonga wapiga kura.
Dkt Ruto alikuwa akimuunga mkono mgombeaji huru Feisal Bader naye Bw Odinga alimpigia upato Bw Omar Boga wa ODM.
Watu kadhaa walijeruhiwa na wengine kukamatwa kufuatia fujo hizo katika vituo kadhaa vya kupigia kura.
Licha ya uchaguzi huo kuvutia idadi ndogo ya wapiga kura, madai ya hongo yalikuwa mengi huku mirengo ya Dkt Ruto na Bw Odinga ikishtumiana.
Kufikia saa kumi na mbili asubuhi upigaji kura ulikuwa umeanza katika vituo vyote 129 bila tatizo, lakini baada ya saa chache ghasia zilianza katika vituo kadhaa.
Vurugu kubwa zilitokea katika kituo cha Mwaroni na kile cha shule ya msingi ya Jomo Kenyatta.
Machafuko katika kituo cha kupigia kura cha Jomo Kenyatta yalipelekea mshirika wa karibu wa Dkt Ruto, aliyekuwa seneta wa Machakos Johnson Muthama kukamatwa kwa madai ya kutatiza amani kituoni hapo.
Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar alisema Bw Muthama alipelekwa katika kituo cha polisi cha Bandari jijini Mombasa.
“Tunakaa macho kwa sababu tunajua wapinzani wetu wanahonga wapiga kura,” alidai Bw Omar.
Kwenye kituo cha kupigia kura cha Jomo Kenyatta, vikundi viligombana baada ya mabishano kuhusu madai ya hongo kwa wapiga kura.
Vikundi hivyo viwili pia vilirushiana mawe na kupelekea kuvunjwa kwa vioo vya magari yaliyokuwa kituoni hapo.
Ugomvi pia ulishuhudiwa katika kituo hicho kati ya aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale dhidi ya Mbunge wa Likoni Mishi Mboko na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.
Viongozi hao wawili wa ODM walidai kwamba Bw Khalwale alikuwa akiwahonga wapiga kura.
KULAUMIANA
Fujo pia zilitokea katika uwanja wa Jogoo ambapo wafuasi wa Bw Bader wakiongozwa na Mbunge wa Nyali Mohammed Ali walikabiliana na wa Bw Boga, kila upande ukishtumu mwingine kwa madai ya kuhonga wapiga kura.
Afisa kutoka Shirika la Kutetea Haki za Waislamu (MUHURI) alidai kuwa mbunge huyo akiandamana na vijana walifika hapo wakiwa kwenye msafara wa magari 10 na kuanza kusababisha fujo.
Walioshuhudia kisa hicho alisema wafuasi wa Bw Bader walichochea ghasia hizo.
Alisema vijana hao walidai kwamba kuna mpiga kura aliyekuwa akiwahonga wenzake.
Malumbano pia yalitokea nje ya kituo cha kupigia kura kati ya Bw Ali na Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir.
Kamanda wa polisi Kaunti ya Kwale Joseph Nthenge alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo.
“Ikiwa mtu aliyevamiwa ameripoti suala hilo kwa polisi basi tutachukua hatua na kuchunguza,” alisema.
Akizungumza na wanahabari baada ya kupiga kura, Bw Boga alishutumu ghasia hizo: “Tunafahamu kuwa wanaleta mvutano katika ngome zangu ili watu wasijitokeze. Ninataka kuwahakikishia watu wangu kuwa hali sasa imedhibitiwa na polisi wametuhakikishia usalama kamili,” akasema Bw Boga katika uwanja wa Jogoo.
Kwa upande wake, Bw Bader ambaye alipiga kura katika kituo cha Gazi alishtumu kundi la Bw Boga kwa madai ya kusababisha machafuko katika shule ya msingi ya Jomo Kenyatta.
Bw Bader alidai wafuasi wa ODM ndio waliosababisha rabsha na kuwatisha wapiga kura.
“Hatutaogopa au kutishwa. Wawaache watu wa Msambweni wachague kiongozi wampendaye. Ninawasihi sisi sote tudumishe amani kwa sababu tunahitajiana hata baada ya uchaguzi mdogo,” alisema.
Kundi la Bw Bader limekuwa likilalamika kuwa maafisa wa usalama wamekuwa wakiwatatiza wakati wa kampeni.