Habari

Ruto: Sitaomba msamaha kwa kujenga kanisa Ikuluni

Na WINNIE ONYANDO July 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amekubali kuwa anajenga Kanisa Ikuluni akidai kuwa anatumia pesa zake kulijenga.

Kiongozi huyo wa nchi alisema kuwa yeye anaamini Mungu na kwamba hataomba masamaha kwa kujenga Kanisa la Mungu.

“Tutajenga kanisa la Mungu, shetani akasirike afanye kile anachotaka,” Rais Ruto alisema.

“Ni kweli mimi najenga Kanisa hapa Ikuluni kwani nilipata kanisa la mabati. Kanisa la mabati inatoshana na Ikulu?

Kwa upande mwingine Dkt Ruto anasema kuwa anatumia pesa zake kujenga hilo kanisa.

“Haitagharimu serikali ya Kenya hata shilingi moja kwani najenga na pesa zangu,” akaongeza Dkt Ruto.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya habari kuhusu ujenzi wa kanisa hilo lenye uwezo wa kusitiri watu 8,000 kufichuliwa kwenye magezeti ya “Taifa Leo” na “Daily Nation”.

Kulingangana na ufichuzi huo, kanisa hilo, lililopambwa kama ‘Cathedral’, linaundwa na Skair Architects Limited na lina madirisha marefu na picha za setilaiti zinaonyesha ujenzi unaoendelea karibu na eneo la kutua helikopta ya Rais.

Ufichuzi huo umekashifiwa vikali na Wakenya katika mitandao mbalimbali ya kijamii huku baadhi wakimkemea Rais Ruto kwa kuharibu pesa za umma.