Habari

Ruto: Upinzani utakuwa mswaki kwangu 2027

Na PIUS MAUNDU November 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto jana alikejeli upinzani, akisema utakuwa mswaki kwake 2027 kwa sababu wanarudia makosa yale yale upinzani ulifanya mnamo 2022.

Kiongozi wa nchi alisema kuwa Muungano wa Upinzani chini ya Vinara wake Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua hauwezi kumshinda kwa kukita siasa zao kwenye ukabila na kugawana mamlaka kupitia mikutano ya faragha hotelini.

“Mnamo 2022 tulionya upinzani dhidi ya kutumia muda wao kugawana mamlaka hotelini na tukawashinda walipokosa kufuata ushauri wetu. Upinzani wa sasa unarudia makosa yale yale ya 2022,” akasema Rais Ruto akiwahutubia viongozi wa mashinani kutoka kaunti za Machakos, Kitui na Makueni kwenye Ikulu ndogo ya Kitui.

Rais amekuwa katika ziara ya siku nne katika eneo la Ukambani ambalo ni ngome ya kisiasa ya Bw Musyoka.

“Badala ya kutuambia jinsi ambavyo watabuni nafasi za ajira kwa vijana na kuimarisha sekta za kilimo, elimu na afya wao ni kusema tu ‘WanTam’ , ‘Kasongo Lazima Aende’,” akaongeza Rais Ruto.

Kiongozi wa nchi alijitapa kuwa uongozi wake umeinua maisha ya Wakenya na bado utaendelea kubadilisha maisha ya Wakenya.
Kauli ya Rais ilikuja siku moja tu baada ya Bw Musyoka kumwonya dhidi ya kumpuuza kisiasa.

“Kalonzo Musyoka si marehemu Raila Odinga ambaye kura zake ziliibwa 2013, 2017 na 2022. Nitaomba sana ili wale ambao wanapanga kuiba kura zangu wachanganyikiwe,” akasema Bw Musyoka.

Kiongozi huyo wa Wiper alilazimika kuingilia kati na kuwatetea Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, Seneta wa Makueni Daniel Maanzo na Mbunge wa Kilome Thaddeus Nzambia ambao waliandamana na Rais katika ziara yake ya maendeleo mnamo Jumatano.

Alisema kuwa mgawanyiko ambao unasukumwa kwenye kambi yake utanufaisha tu mrengo wa Rais Ruto na kuuzolea uungwaji mkono Ukambani.
Bw Musyoka alikariri kuwa licha ya miradi ya maendeleo ambayo ilizinduliwa kwenye ziara ya Rais Ruto, bado eneo hilo lenye wapigakura milioni 1.7 litamuunga mnamo 2027.

Kati ya miradi ambayo Rais Ruto alianzisha ni kuwekwa lami kwa barabara ya Emali-Ukia Kaunti ya Makueni.

“Tumewekeza Sh110 bilioni katika miradi mbalimbali kaunti za Kitui, Machakos na Makueni. Kati ya pesa hizi Sh64 bilioni zitakuwa za kujenga nyumba za gharama nafuu, vyumba vya malazi 15,000 kwa wanafunzi na masoko 39 ya vyakula,” akasema Rais Ruto.

“Miradi hii itabuni nafasi za kazi na kuimarisha maisha. Tunaweka lami katika zaidi ya kilomita 600 za barabara kwa kima cha Sh30 bilioni ili kuimarisha biashara na kufungua eneo hili kiuchumi,” akasema Rais.

Kulikuwa na sherehe na shangwe pamoja na tafrija Rais Ruto alipowapa wamiliki 176 wa nyumba funguo mjini Machakos. Hii ni baada ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kukamilika eneo hilo.