Ruto, wandani watumia mazishi ya Injendi kuponda wanahabari kuhusu ukosoaji wa serikali
VYOMBO vya habari vilijipata pabaya wakati Rais William Ruto na wandani wake walipowashutumu wanahabari kwa kueneza habari za uongo na kuvuruga ukweli kuhusu sera na miradi ya serikali.
Rais William Ruto ameshutumu vyombo vya habari kwa kutumiwa na wakosoaji wake kusambaza habari feki na kuvuruga ukweli kuhusu ajenda ya serikali yake kuhusu maendeleo kupitia vituo vya habari na mitandao ya kijamii.
Akizungumza wakati wa mazishi ya marehemu mbunge wa Malava, Malulu Injendi, Dkt Ruto alionya kuwa tabia hiyo huenda ikahatarisha uhuru, demokrasia na maendeleo ya nchi.
“Japo kuna nafasi ya mdahalo, ukosoaji na mapendekezo mbadala, sehemu kubwa ya kinachotangazwa kama ukweli kuhusu miradi ya serikali ni uongo, na pingamizi nyingi zinatokana na vyombo vya habari kuvuruga ukweli,” alisema Dkt Ruto.
Alitaja Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) inayokabiliwa na pingamizi kali kutoka ngome zote za kisiasa akisema Wakenya wanashindiliwa uongo kuhusu mpango huo na vyombo vya habari.
Alisema serikali yake imeweka msururu wa kampuni za kiteknolojia kudhibiti ulaghai uliokithiri katika Bima ya Afya Kitaifa (NHIF) ili usijitokeze katika SHA.
“Wanaolalamika kuhusu SHA ni watu ambao wamekuwa wakipora bima ya afya. Nataka kuwaeleza wizi sasa umeisha. Hata mkijaza kurasa laki moja za magazeti kushinikiza kurejea kwa NHIF, haitofanyika,” alisema.
Alisema Kenya Kwanza imejitolea kuhakikisha huduma bora ya afya kwa bei nafuu sio kwa watu wahache bali inafurahiuwa na Wakenya wote jinsi inavyoagizwa kikatiba.
Kauli yake ilisisitizwa na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah na mwenzake katika Seneti, Aron Cheruiyot.
Bw Mudavadi aliagiza vyombo vya habari kuwa na nidhamu katika utangazaji wake na kusuuza ukweli kutoka kwenye uongo.
“SHA na Nyumba za Bei Nafuu ni miradi bora zaidi kuwahi kuanzishwa nchini. Lakini inasawiriwa kama miradi mibaya na vyombo vyetu vya habari. Tuwe na nidhamu tunaporipoti na kusaidia serikali yetu kusonga mbele,” alisema Bw Mudavadi.
Bw Wetang’ula aliwahimiza Wakenya wasiamini ripoti zinazodhamiriwa kuharibu ajenda ya serikali kuhusu maendeleo.
Alisema wanaolalamika dhidi ya SHA sio wanachama waliojisajili na hawaelewi jinsi mfumo huo unavyofanya kazi lakini wanaamini ripoti za kupotosha kutoka kwa vyombo vya habari.
“Usiamini ripoti kwamba SHA haifanyi kazi. Jisajili na uzuru kituo cha afya. Hapo ndipo utagundua umuhimu wa mpango huu. Achana na unachoona na kusikia kutoka kwa vyombo vya habari,” alisema.
Bw Ichung’wah alitoa wito kwa Wakenya kutilia maanani huduma ya afya yao pasipo kusikiza uzushi unaosambazwa kupitia vyombo vya habari “vinavyopotosha kuhusu SHA”.