Habari

Sababu alama halisi za KJSEA kusalia siri

Na DAVID MUCHUNGU Na MERCY SIMIYU December 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUTANGAZWA kwa matokeo ya Tathmini ya Elimu ya Shule ya Sekondari Msingi Kenya 2025 (KJSEA) Desemba 11, 2025 ni hatua muhimu katika mtaala wa elimu unaozingatia umilisi ( CBE).

Kwa kuwa ni mtihani wa aina hii wa mara ya kwanza, wanafunzi wengi, walimu na wazazi wanatarajia kuona jinsi watahiniwa watakavyopatiwa alama na matokeo kupangwa.

Watahiniwa 1.1 milioni waliofanya mtihani huo watapewa matokeo yao kwa mfumo tofauti na ule ambao nchi imezoea.

Hakutakuwa na alama za asilimia, badala yake matokeo yatakuwa maelezo ya ubora ikifuatiwa na alama ya namba.

Kila somo litapewa alama ya juu ya 8 na kutokana na masomo tisa yaliyotahiniwa, alama ya juu kabisa ambayo mtahiniwa anaweza kupata ni 56.

Hivyo basi, itakuwa vigumu kupanga watahiniwa kulingana na asilimia zao jumla.

Asilimia halisi ya alama haitafichuliwa kwake, lakini itatumika kumweka katika makundi ya utendaji (Kupitisha Matarajio, Kutimiza Matarajio, Kukaribia Matarajio na Chini ya Matarajio).