Habari

Sababu nane za Rigathi kuunga Kalonzo debeni

Na MWANGI MUIRURI December 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KATIKA kile kinachoonekana kuwa juhudi za kumtangaza kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kama mgombeaji urais anayeungwa na Mlima Kenya, chama cha DCP kimetaja sababu nane zinazomfanya kuwa mwanasiasa wa kuvutia.

Ingawa wote wawili – Bw Musyoka ambaye ni makamu rais wa 10 na Bw Rigathi Gachagua aliye naibu rais wa pili, wamewahi kushikilia wadhifa wa pili kwa ukubwa serikalini, kwa sasa ni vinara wenza ndani ya muungano wa upinzani .

Vinara wengine ndani ya muungano huo ni naibu kiongozi wa Jubilee, Dkt Fred Matiang’i; kiongozi wa DAP-K, Bw Eugene Wamalwa; Kiongozi People’s Liberation Party, Bi Martha Karua; na Gavana wa Trans Nzoia, Bw George Natembeya.

Hata hivyo, matamshi ya Bw Gachagua hadharani yanaashiria mtu anayefanya kampeni za urais akiwa na nia ya kumuunga Bw Musyoka.Anasisitiza kuwa Bw Musyoka ana sifa zinazomfanya kuwa mtu muhimu kwa muungano.

“Nina uhakika Bw Musyoka hawezi kusaliti Kenya, watu wake na watu wangu ni familia kisiasa. Si mjinga asiyefahamu umuhimu wake kwa sasa. Tuna makubaliano, ni mwathiriwa kama mimi na ana tajriba ya miaka 15 ya kujaribu kuondoa serikali madarakani,” asema Gachagua.

Sifa nyingine ni kuwa Bw Musyoka “anaweza kutusaidia kupata sura kitaifa kwa kushirikisha ODM kama washirika wetu na zaidi ya yote, Bw Musyoka ni mtu anayeaminika asiyeweza kukiuka makubaliano.”

Mbinu ya Bw Gachagua kumpigia debe Bw Musyoka inaeleza safari ngumu ambayo upinzani utalazimika kupita kuelekea 2027.

Mchanganuzi wa siasa Gasper Odhiambo anasema kuwa kudumisha umoja wa vyama vidogo na vinara wao, kujenga muafaka wa kumpata mgombeaji wa pamoja wa urais, na kushughulikia kero ya kura za mchujo wa pamoja katika kaunti, maeneobunge na wadi ni baadhi ya changamoto kuu.

Hii ni pamoja na ufadhili wa kampeni, kukabiliana na ukali wa serikali iliyo madarakani, usajili wa vijana wa Gen Z kama wapiga kura, na hata kuwashawishi wajitokeze kupiga kura na kuunga mkono upinzani.

“Tusisahau mirengo mipya ya kisiasa kama Kenya Moja ambayo ina “mabawa” yaliyotoka serikalini na upande wa upinzani,” anasema.

Katika hotuba yake akiwa katika Kaunti ya Murang’a majuzi, Bw Gachagua alisema kuwa amejikita kwenye hesabu zitakazohakikisha Rais Ruto anahudumu kwa muhula mmoja.

“Ningeogopa sana iwapo siasa haingekuwa mchezo wa idadi ya wafuasi. Mwisho wa siku ni kura ngapi zitaanguka upande wako. Kushinda ni kuunganisha ushindi,” akasema.

Hii ilitanguliwa na matamshi yake ya hivi majuzi kuwa ana makubaliano na Bw Musyoka kuachia DCP uongozi wa Nairobi.

Mnamo Desemba 9 2025, akiwa Murang’a, Bw Musyoka alisema: “Bw Gachagua huwa muungwana katika ukweli na napenda jinsi anavyorahisisha mambo magumu.”

Katika ibada ya shukrani katika Kanisa la Dominion City, Kasarani, Kaunti ya Nairobi, Jumapili iliyopita, Bw Gachagua alisisitiza kuwa “safari hii inahitaji utaalamu wa Musyoka.”

Kwa mujibu wa Bw Gachagua, kumshinda Rais William Ruto mwaka 2027 “kutahitaji zaidi ya kauli mbiu na majivuno… kutahitaji mgombea thabiti, muungano imara, uwezo wa kuthibitisha ushawishi wa wapiga kura na kuweza kugeuza jitihada kuwa kura za kuzuia aliye madarakani kurejea.”

Katika matamshi yake hadharani, Bw Gachagua amekuwa akisema kuwa “Mlima Kenya unaweza kutoa kura milioni saba hadi nane ilhali Ukambani inaweza kutoa kati ya milioni tatu na nne… hizi ndizo takwimu za kitaifa.”

Tangu uchaguzi wa vyama vingi wa 2002, Bw Musyoka amethibitisha uwezo wa kuongoza ngome yake kupiga kura kwa mwelekeo anaotaka.

Hata alipodhalilishwa 2022 alipoondolewa kama mgombea mwenza wa Bw Raila Odinga na nafasi yake kutwaliwa na Bi Karua, Bw Musyoka aliweza kushawishi ngome yake kumpigia kura Bw Odinga.

Wachambuzi wa siasa wanaamini kuwa Bw Musyoka ana kile anachotafuta Bw Gachagua: uwezekano mkubwa wa kusikilizwa na ngome yake na kuwapa mwelekeo wafuasi wake.

“Iwapo Bw Gachagua atafanikiwa kuvuta kura za Mlima Kenya upande wake na Bw Musyoka afanikiwe vivyo hivyo Ukambani, huo utakuwa muungano mgumu kushindwa kwani utavutia kura kutoka kwa vikundi vingine vidogo,” asema Bw Odhiambo.