Habari

Sababu ya Safaricom kukawia kuzima nambari za malipo za kampuni za kamari

July 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KAMPUNI ya huduma za mawasiliano ya Safaricom imesema itahitaji muda kutekeleza amri ya kuzima nambari za malipo za kampuni za kamari ambazo zilipokonywa leseni za kuhudumu.

Mawakili wake Alhamisi waliiambia Bodi ya Kudhibiti Michezo ya Kamari Nchni (BCB) kuzima nambari hizo za malipo mara moja kutawasababishia hasara mamilioni wa watumiaji ambao tayari wameweka pesa zao katika kampuni kadha za kamari.

“Amri hiyo ya bodi hiyo itaathiri zaidi ya wateja 12 milioni,” Safaricom ikasema.

Kampuni hiyo ya mawasiliano iliongeza kuwa kampuni mbili za kamari zilikuwa zimepata agizo la mahakama la kuziruhusu kuendelea na shughuli zao bila kuchukua upya leseni za kuhudumu.

Wakuu waa Safaricom ambao hawakutaka kutajwa majina walisema kuwa katika miaka ya hivi karibuni sekta ya kamari imekuwa ikiiletea mapato mengi zaidi.

Kampuni hii hasa huingiza mapato kupitia hudumu za ujumbe mfupi (sms) na M-Pesa.

Mnamo Jumatano serikali kupitia bodi ya BCB iliziamuru kampuni 27 zilizopigwa marufuku kwa kukoa kitimiza masharti yaliyowekwa, hususan, ulipaji ushuru.

Kampuni ambazo ziliathirika ni kama zifuatazo:

  1. SportPesa
  2. Betin
  3. Betway
  4. Betpawa
  5. Elitebet
  6. PremierBet
  7. Lucky2u
  8. 1xBet
  9. MozzartBet
  10. Dafabet
  11. World Sports Betting
  12. Atari Gaming
  13. Palms Bet
  14. Betboss
  15. Kick-Off
  16. Millionaire Sports Bet
  17. Cheza Cash
  18. Betyetu
  19. Bungabet
  20. Cysabet
  21. Saharabet
  22. Easibet
  23. Easleighbet
  24. Sportybet
  25. AGB lottery and gaming
  26. Atari
  27. Kickoff

Kampuni za kamari zinazoendesha shughuli zake mitandaoni kama vile SportPesa imenawiri zaidi nchini Kenya na katika mataifa jirani katika miaka karibuni.

Hii ni kwa sababu watu wengi hupenda kubashiri matokeo ya mechi, hasa zile za kigeni.

Hali hii, kwa mfano,  ilipelekea kampuni hiyo kukusanya mapato ya kima cha Sh204 bilioni mwaka jana.

Kampuni za kamari hutegemea umaarufu wa Safaricom katika sekta ya mawasiliano kuwezesha wateja wake kucheza, wao kuwasiliana na wateja wao na kuandaa na kuwasilisha malipo kupitia huduma za kupokea na kutuma fedha, kama vile M-Pesa.