Sababu za Kenya kung'ang'aniwa kama mpira wa kona
WYCLIFFE MUIA na PETER MBURU
MATAIFA yenye uwezo mkubwa kiuchumi kutoka Magharibi na Mashariki mwa ulimwengu yameonyesha kuvutiwa zaidi na bara Afrika siku za hivi majuzi, Kenya ikimulikwa na yote katika hatua zao za awali za kupata posho kubwa la uwekezaji.
Yakiongozwa na Marekani, Uingereza na Uchina, mataifa haya yamezidi kuonyesha kuwa yanahitaji ushirikiano zaidi na Kenya, viongozi wake wakijitokeza waziwazi na kutoa ahadi maradufu, hali inayofanya Kenya kuonekana kama mpira wa kona kwenye kisanduku cha penalti katika mechi ya soka.
Kuongezeka kwa ziara za viongozi wa mataifa hayo humu nchini ama mialiko kwa Rais Uhuru Kenyatta kuelekea kwayo kufanya mikutano ya kibiashara kumeonyesha namna Kenya inavyochangamkiwa.
Kwa mfano, katika kipindi cha mwezi mmoja pekee, Rais Kenyatta atakuwa amekutana na viongozi wa nchi hizo tatu ambazo zote ni mashujaa wa kiuchumi ulimwenguni.
Wiki iliyopita, alizuzuru Marekani na kufanya kikao na Rais Donald Trump, Alhamisi akampokea Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na Jumamosi aliwasili Beijing, Uchina, kuhudhuria Kongamano la mwaka huu la Ushirikiano wa China-Afrika (FOCAC).
Wachanganuzi wa uchumi-siasa wanahusisha mvuto huo na ushawishi mkubwa wa Kenya katika kanda ya Afrika Mashariki na kuendelea kuwa kitovu cha masuala ya kiuchumi, kisiasa, kiteknojia na kidemokrasia barani.
“Kwa mfano, Shirika la BBC limefungua afisi yake kuu ya Afrika nchini Kenya kwa sababu ya umuhimu wa Kenya barani. Hii inaonyesha kuwa licha ya kuwepo changamoto nchini, Kenya bado ni kiungo kikubwa barani,” anasema Dismus Kimilu, mtaalamu wa kiuchumi.
Mbali na BBC, duka kubwa la Ufaransa, Carrefour limeanzisha matawi yake nchini Kenya. Vilevile duka kubwa la Massmart linalomilikiwa na Walmart, ya Afrika Kusini pia limetua Kenya na kuzidisha ushindani wa kibiashara nchini.
Duka kubwa nchini Botswana, Choppies, vilevile limenunua matawi 10 ya maduka ya kijumbla ya Ukwala, hatua ambayo imetishia maduka ya Tuskys na Naivas. Kenya imeanza kupanua mbawa zake katika Afrika Magharibi ili kufikia masoko ya eneo hilo na kupata ushawishi zaidi wa kiuchumi kanda hiyo.
Kulingana na stakabadhi za kigeni zilizoonekana na Taifa Jumapili, Kenya inataka kuwa na ushawishi katika Jumuiya ya Kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas), yenye wanachama 15, kwa kufungua balozi zaidi eneo hilo.
Kwa sasa Kenya ina ubalozi mmoja tu mjini Abuja, Nigeria na inapanga kufungua mabalozi zaidi katika mataifa ya Ghana, Senegal na Mali.
Bw Kimilu anasema ili mataifa yenye nguvu duaniani kuwekeza barani Afrika sharti yapitie Kenya kwa sababu ya ushawishi wake.
Alipokutana na Rais Trump wa Marekani, viongozi hao walizungumzia masuala muhimu ya kibiashara, huku akitoka huko na biashara za uwekezaji za takriban Sh23bilioni kutoka kwa kampuni tatu katika sekta za kawi na kilimo.
Viongozi hao walizungumza kuhusu mbinu za kuimarisha biashara, uwekezaji na usalama baina ya mataifa yote mawili, mbali na kujadili namna wawekezaji kutoka Amerika watakavyoweza kufanya biashara humu nchini katika mazingira bora zaidi, bila matatizo.
“Kenya na Marekani zimekuwa na uhusiano dhabiti tangu tupate uhuru, tuko hapa kuimarisha ushirikiano huo. Tumekuwa na ushirikiano mzuri haswa katika vita dhidi ya ugaidi,” akasema Rais Kenyatta. Rais Kenyatta alieleza kuwa idadi kubwa ya kampuni kutoka Marekani zinazofanya biashara Kenya zimesaidia kupanua maendeleo, huku naye Rais Trump aliahidi kutimiza ‘mazuri’ kwa Kenya
“Tunaenda kumalizia vitu vingi vizuri, tutafanya dili nzuri kwa mataifa yote mawili,” akasema Rais Trump.
Ziara ya Rais Kenyatta ilikuja siku chache baada ya kampuni moja ya Marekani kutangaza kufadhili ujenzi wa barabara kuu ya Nairobi-Mombasa, itakayogharimu Sh300bilioni.
Naye Bi May alipofika katika ikulu ya Nairobi Alhamisi, alifika na ahadi za kuzidisha ushirikiano kati ya Kenya na Uingereza, kutoa pesa za kusaidia wanajeshi wa Amisom walioko Somalia na kuimarisha usalama maeneo ya mipakani na kusaidia Kenya kurejesha pesa za ufisadi zilizofichwa katika nchi yake.
Hii ilikuwa licha ya ahadi kuwa hata baada ya Uingereza kujiondoa kutoka muungano wa mataifa ya bara Uropa (EU), biashara kati ya Kenya na UK hazitaadhiriwa.
“UK ndilo taifa la nje lililowekeza sana Kenya na ni lengo letu kuwa mwekezaji mkubwa barani Afrika kati ya mataifa ya G7. Hata Uingereza inapojiandaa kuondoka EU, tumejitolea kuwa na mpito mzuri na kuendeleza ushirikiano wa kibiashara,” akasema Bi May.
Kulingana na utafiti wa mwaka huu Kenya ilisambazia UK bidhaa za Sh38.55 bilioni mwaka uliopita, huku majani chai, maua na maharagwe yakiongoza orodha ya bidhaa zilizouziwa nchi hiyo. Katika kipindi hicho, kenya ilinunua bidhaa za Sh30bilioni kutoka Uingereza.
“Biashara kati yetu na Uingereza inatufaa zaidi yao na hivyo tunataka kuzidisha hali hiyo,” akasema waziri wa masuala ya nje Dkt Monica Juma.
Vilevile, Uingereza ndiyo huleta watalii wengi zaidi humu nchini, huku mwaka jana raia wake 168,000 wakiwa walizuru Kenya, kati ya nusu milioni kutoka Uropa kipindi hicho.
Wakati Rais Kenyatta akitia juhudi kuwacha sifa ya kumaliza ufisadi na kuleta maendeleo kulingana na ajenda nne kuu alizoorodhesha kuwa nguzo zake za kipindi hiki, mataifa hayo yanatumia nafasi hiyo kujilainisha na malengo yake ili kupata nafasi kupenyeza.
“Kenya imejitolea kufungua nafasi za biashara kwa wote na si kwa kukopa ila kwa kuandaa nafasi za uwekezaji ili kampuni za nje zije,” Rais Kenyatta akasema.
Miezi mitatu baada ya kutia saini mkataba na serikali ya Uswizi ili pesa zilizofichwa na wafisadi katika benki za nchi hiyo zirejeshwe Kenya kufanya maendeleo, Alhamisi aliingia katika mkataba sawia na Uingereza ili mali na pesa za umma zilizoibiwa zirejeshwe.
Wiki ijayo, Rais Kenyatta anatarajiwa kusafiri kuelekea Beijing, Uchina kukutana na Rais Xi Jinping kwa mazungumzo kuhusu namna ya kuzidisha ushirikiano wa kibiashara na taifa hilo ambalo mwongo uliopita limeshika karibu sekta zote za ujenzi humu nchini.
Nyingi za barabara zinazojengwa na zilizojengwa miaka ya hivi majuzi zimekuwa zikijengwa na kampuni kutoka Uchina, huku nchi hiyo ikizidisha ushirikiano hata katika ngazi za kisiasa.
Balozi wa Uchina Kenya Bi Sun Baohong alisema nchi yake iliamua kushirikiana katika sekta zenye umuhimu kama elimu na teknolojia ambazo mataifa haya mawili yanaweza kushirikiana.
Kenya ni moja ya mataifa manne barani ambayo Uchina imebaini ya kuanzisha vituo vya ujenzi wa viwanda, huku ikiwa mkopeshaji mkubwa wa taifa hili kwa deni la Sh534bilioni.
Mataifa mengine kama Israili aidha yameonyesha kutafuta ushirikiano na Kenya kwani Waziri Mkuu wa huko Benjamin Netanyahu alitembea mwaka uliopita.