Sababu za Ruto kutuma kikosi maalumu cha KDF kuzima wezi wa mifugo
RAIS William Ruto ametangaza mpango wa kupeleka upya kikosi maalum cha Special Operations Group (SOG) katika eneo la Baragoi, Kaskazini mwa Samburu kukabiliana na wezi wa mifugo.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya siku mbili katika Kaunti ya Samburu, Rais Ruto alisema serikali yake imejitolea kuhakikisha amani ya kudumu inarejea katika eneo hilo ambalo limekuwa likikumbwa na mauaji na mapigano kwa miongo kadhaa.
“Kama serikali, hatutaendelea kupoteza maisha ya Wakenya wasio na hatia mikononi mwa wahalifu. Hatutakoma hadi kila bunduki haramu itakaposalimishwa na amani kurejea Baragoi na maeneo yote ya Kaskazini mwa Kenya,” akasema Dkt Ruto.
Baragoi imekuwa ikijulikana kwa mapigano ya mara kwa mara yanayosababishwa na wizi wa mifugo miongoni mwa jamii za wafugaji kwa zaidi ya miaka 40.
Katika wiki za hivi karibuni, ripoti zimeonyesha kurejea kwa uvamizi wa wezi wa mifugo na mashambulizi katika maeneo ya Suyian, na kando ya barabara za Baragoi–Tuum na Baragoi–South Horr.
Rais Ruto alitoa wito kwa wale wanaomiliki silaha haramu kuzisalimisha, akionya kuwa serikali haitaruhusu matumizi ya bunduki kuendeleza uhalifu. Alifichua kuwa mashirika ya usalama yamewatambua watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na watakabiliwa vikali iwapo hawatazirejesha kwa hiari.
“Ikiwa unajua rafiki yako ana bunduki, mwambie alete haraka kabla hatujamtembelea. Hizo ndizo chanzo cha mauaji katika Baragoi,” alisema Rais.
Dkt Ruto alisema visa vya matumizi ya silaha katika eneo hilo vimeacha majonzi, uharibifu wa mali na familia nyingi zenye wajane na mayatima.
Kikosi maalum cha SOG, kilichoundwa kutoka wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), vilitumwa hapo awali miaka miwili iliyopita kusaidiana na Kikosi cha Kukabiliana na Wizi wa Mifugo (ASTU) na Kitengo Kukabiliana na Dharura (RDU) katika kupambana na wizi wa mifugo unaokumba eneo hilo.
Gavana wa Samburu, Lati Lelelit, alikiri kuwa vikosi hivyo vilifanya kazi nzuri katika kurejesha utulivu wa muda mrefu katika Baragoi, eneo lililokuwa likisumbuliwa na wizi wa mifugo kwa miaka mingi.
Rais Ruto amesisitiza mara kadhaa kwamba Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) litabaki katika maeneo yanayokumbwa na uhalifu wa wizi wa mifugo Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Amesema mbali na kurejesha hali ya kawaida, maafisa wa jeshi pia watahusika katika miradi ya maendeleo ya jamii ili kufungua eneo hilo kiuchumi.