Habari

SADC yahimiza mataifa 16 wanachama wapigie mwaniaji wa Madagascar, sio Raila

Na FATUMA BARIKI February 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

UONGOZI wa Jumuiya ya Muungano wa Kiuchumi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) umetaka wanachama wake 16 wapigie kura mwaniaji wa Madagascar katika uchaguzi wa Tume ya Umoja wa Afrika, (AUC) Februari 15.

Sekretarieti hiyo inataka wanachama hao wamchague Richard Randriamandrato ikisema ni mwenzao, jambo lililomaanisha kwamba haishabikii tiketi ya mwaniaji wa Kenya, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Hata hivyo, Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni Korir Sing’oei anashikilia kwamba wana imani kubwa Bw Odinga ataibuka mshindi katika uchaguzi huo wa Jumamosi.

Haya yanajiri huku zikiwa zimebaki saa za kuhesabu kabla ya kura hiyo inayosubiriwa kwa hamu nchini Kenya kutokana na athari za siasa za ndani ya nchi ambazo zinaweza kutokea kufuatia kushinda au kushindwa kwa Raila katika kura hiyo.

Kwa kipindi kirefu, mwaniaji wa Djibouti, Waziri wa Mashauri ya Kigeni nchini humo Mahmoud Ali Youssouf, alichukuliwa kuwa mshindani mkuu wa Raila ambaye amefanya kampeni kabambe, kwa usaidizi mkubwa wa serikali ya Rais William Ruto.

Bw Youssouf anaaminika kuwa na uungwaji kutoka mataifa yanayozungumza Kiarabu na Kifaransa kutokana na lugha hizo kuwa miongoni mwa zinazozungumzwa nchini Djibouti.