Habari

Sakaja alala kituoni baada ya kukamatwa katika baa wakati wa kafyu

July 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Nairobi Johnson Sakaja Ijumaa saa saba za usiku alikamatwa na polisi katika baa moja mtaa wa Kilimani kwa kukiuka masharti ya kafyu.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumamosi asubuhi, afisa mmoja wa polisi alipata habari kwamba baa moja kwa jina Ladies Lounge iliyoko kando ya barabara ya Dennis Pritt ilikuwa ikiendelea na hudumu mwendo wa saa saba na dakika 10.

Alipofika katika baa hiyo, afisa huyo alimpata Seneta Sakaja akiwa pamoja na watu wengine 10 wakibugia pombe nje.

Seneta Sakaja aliamriwa aondoke lakini akadinda. Hivyo, afisa huyo alimwita mwenzake kwa jina Asambasa, wa cheo cha Sajini ambaye pia alishindwa kumshawishi Sakaja aondoke.

Baadaye Naibu Afisa Mkuu wa Polisi Adan Hassan na maafisa wengine walifika pahala hapo.

“Hapo ndipo Mheshimiwa Sakaja akaanza kuzua fujo. Aliwachochea wenzake wasiondoke pahala hapo, ingawa baadhi yao walikuwa tayari wametoroka, na hapo ndipo akatiwa mbaroni,” ripoti hiyo ikasema.

Akiwa katika korokoro ya polisi, Sakaja aliambiwa aachiliwa kwa dhamana lakini akataa kuondoka. Alitisha kuhakikisha kuwa maafisa wote katika Kituo cha Polisi cha Kilimani wamehamishwa “ndani ya saa 24.”