HabariHabari za Kitaifa

Sakaja atupa Wilbaro, alenga kujinafasi 2027 kupitia ODM

Na KEVIN CHERUIYOT November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja jana alijiunga rasmi na chama cha ODM akilenga kuimarisha nafasi yake ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao.

Bw Sakaja, aliyechaguliwa mnamo 2022 kwa chama tawala cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto, alisema yuko tayari kufanya kampeni za muhula wa pili wa Rais akiwa mwanachama wa ODM.

ODM na UDA kwa sasa ziko katika Serikali Jumuishi, huku zikiendelea na mchakato wa kutia saini mkataba wa ushirikiano kabla ya uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, hafla ya kumpokea Bw Sakaja katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, ilizua hisia tofauti. Gavana huyo alisisitiza kuwa amekuwa akitekeleza matakwa ya aliyekuwa kiongozi na mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga.

“Nilianza safari hii na Baba (Raila Odinga) nilipotwaa ugavana. Na nimekuwa nikishambuliwa kwa kusimama naye na kuwasaidia wanachama wa ODM kuingia katika Baraza la Mawaziri. Nilifanya hivyo kabla ya kuundwa kwa Serikali Jumuishi na Baba ndiye aliyeniambia niingie ODM,” akasema Bw Sakaja.

Bw Sakaja alipokelewa na Naibu Kiongozi wa ODM aliye pia Gavana wa Kisii, Simba Arati, Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama hicho na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Mbunge wa Suna Mashariki na Mkurugenzi wa Uchaguzi ODM Junet Mohammed, pamoja na Waziri wa Madini Hassan Joho.

Gavana huyo alisema anajiunga na chama hicho kwa unyenyekevu, akiwa tayari kuongozwa na ngazi zake za juu na kuanza kampeni za kuvumisha umaarufu wake.

“Ninaamini kuwa hatua inayofuata ya siasa zetu haipaswi kupimwa tu kwa uchaguzi tunaoshinda, bali pia kwa maisha tunayobadilisha. Vijana hawapaswi tena kuwa watazamaji katika maamuzi yanayoathiri mustakabali wao bali anapaswa kushiriki, kuwa viongozi na kuwa kiini cha Kenya tunayoijenga,” akasema.

Bw Sakaja alikumbushwa kuwa Mwenyekiti wa ODM utanzu wa Nairobi ambaye ni Mbunge wa Makadara George Aladwa pia anawania tiketi ya chama hicho kugombea ugavana wa Nairobi.

“Tuna mwenyekiti wetu wa chama Nairobi, George Aladwa, ambaye amekuwa akisimama na chama kwa muda mrefu na pia anawania kiti cha ugavana kupitia ODM. Sasa tunaye Gavana Sakaja,” akasema Bi Wanga, akiongeza kuwa kila anayetaka kujiunga na chama hicho anakaribishwa.

Jana, Bw Aladwa alisema yuko imara ndani ya ODM na kuwataka wafuasi wake wawe watulivu akisisitiza nia yake ya ugavana bado upo hai.

“Wafuasi wangu nawaelewa lakini tusipoteze muda kutokana na uvumi unaoendelea. Safari ya kuimarisha Nairobi itaamuliwa na raia kwa usawa na haki na demokrasia. Tuendelee kudumisha amani,” akasema Bw Aladwa.

Wakati wa kumpokea Bw Sakaja, Bi Wanga alitangaza kuwa uteuzi wa wagombea utafanywa kwa uwazi na bila ubaguzi.

Bw Arati pia alifichua kuwa Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri ni miongoni mwa wanaotaka kujiunga na ODM ili kuwania kiti hicho hicho.

“Mwenyekiti wetu wa Nairobi, Aladwa, pia anawania ugavana. Atachuana na Gavana Sakaja kuwania tiketi ya chama. Karauri akiamua kujiunga nasi, tutampokea kama tulivyompokea Sakaja. Tunachowaahidi wanachama wetu ni uteuzi huru, wa haki na uwazi,” akasema Bw Arati.

Kutokana na kutokuwepo kwa Bw Aladwa katika hafla hiyo, Bw Sakaja alisema atamtafuta binafsi ili kuunganisha kura za ODM Nairobi na kuhakikisha chama hicho kinashinda viti vingi.

Baadhi ya madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi waliohudhuria hafla hiyo walikuwa wamemuidhinisha Bw Aladwa awali kuwania uongozi wa kaunti hiyo.

Polisi nao walilazimika kutumia vitoza machozi kutawanya kundi la wanachama waliokuwa wakijaribu kuvuruga hafla hiyo. Baadhi yao walisikika wakipiga kelele, “Kama hakuna Aladwa, hakuna ODM.”

Mbali na Gavana Sakaja na Aladwa, ODM inakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wa makundi mengine ambao wametangaza nia ya kuwania kiti hicho.

Wao ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino (chama cha Mwananchi), Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya (DCP) na Askofu Margaret Wanjiru .

Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua pia ametangaza kuwa chama chake cha DCP kinataka kutawala siasa za Nairobi na inaaminika anamuunga mkono Bw Gakuya.