Habari

Sakaja: Nimesimamisha maafisa waliomwaga taka lango la Stima Plaza huko Ngara

Na KEVIN CHERUIYOT March 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja amefichua kuwa serikali yake imewasimamisha kazi maafisa wawili kwa kuamuru kumwagwa kwa takataka nje ya jumba la Stima Plaza lililoko Ngara, Nairobi wiki jana.

Bw Sakaja aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Usalama jana kwamba maafisa hao wanaaminika kuamuru madereva wa malori kumwaga takataka nje ya jengo ambako kuma makao makuu ya kampuni ya kusambaza umeme nchini (KPLC).

Serikali ya kaunti ya Nairobi imekuwa ikuvutana na KPLC kuhusu malimbikizi ya bili ya stima ya kima cha Sh3 bilioni hali iliyolazimu kampuni hiyo kukata umeme katika afisi hiyo wiki moja iliyopita.

Jumatatu, Bw Sakaja aliiambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi kwamba waliosimamishwa kazi kutokana na tukio hilo ni naibu mkurugenzi wa kitengo cha ukusanyaji madeni James Sankale Lempaka na kaimu mkurugenzi wa idara ya Usimamizi wa Mapato John Ntoiti.

Majitaka

Hata hivyo, Bw Sakaja aliiambia kamati hiyo kwamba maafisa wake hawakuhusika na mafuriko ya majitaka nje ya jumba la Electricity House katikati mwa jiji la Nairobi.

Alidai kuwa bomba la majitaka katika jengo hilo lilipasuliwa kimakusudi ili lawama zielekezwe kwa serikali ya kaunti ya Nairobi.