Sakata ya ulaghai wa Sh6.2bn serikalini yachunguzwa
SERIKALI imeanzisha shughuli ya kuwahesabu wafanyakazi katika utumishi wa umma ana kwa ana kufuatia uchunguzi wa madai ya ulaghai wa Sh6.2 bilioni kupitia mfumo wa ulipaji mishahara ya serikali.
Shughuli hiyo itaanza katika Wizara ya Elimu na linalenga kubaini wafanyakazi hewa, ajira zisizo halali na dosari katika rekodi za wafanyakazi wanaolipwa na serikali.
Hatua hiyo inafuatia ukaguzi uliofichua visa vya wafanyakazi wanaodaiwa kushiriki akaunti za benki, rekodi za ajira zisizoaminika na mishahara kulipwa kwa watu ambao hawana taarifa halali za akaunti za benki.
Katika ilani ya Oktoba 16, 2026, Katibu katika Wizara ya Elimu, James Kianda aliwaagiza wakuu wa idara kuhakikisha wafanyakazi wote walio chini yao wanahesabiwa ana kwa ana.
Wafanyakazi walitakiwa kufika katika majengo ya Jogoo House kuanzia Oktoba 19 hadi Jumatano wakiwa na vitambulisho vya kitaifa, vyeti vya nambari ya siri (PIN) vya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA), barua zao za kwanza za ajira na barua za sasa za uteuzi.
Shughuli hiyo itawahusisha wafanyakazi wote, wakiwemo waliolazwa hospitalini na walio katika likizo ya mwaka, ugonjwa, uzazi au likizo nyingine zilizoidhinishwa.
Bw Kianda alionya kuwa mishahara ya wafanyakazi ambao hawatathibitishwa katika zoezi hilo itasitishwa. Alisisitiza kuwa maagizo hayo ni ya lazima na yanapaswa kutekelezwa bila kuchelewa.
Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku alisema uchunguzi uliofanywa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) umewahusisha wasimamizi 84 wa wafanyakazi katika Idara ya Magereza, Huduma ya Polisi na Wizara ya Afya na ukora wa ulaghai kuhusu ulipaji wa mishahara.
Maafisa hao wanadaiwa kuhusika katika udanganyifu wa mishahara na kutokana na hilo wamepokonywa haki ya kuingia katika mfumo wa malipo na kuagizwa kujitenga na majukumu yao kwa siku 30 za kazi ili kuruhusu uchunguzi kuendelea.
Serikali imewateua maafisa wengine kusimamia majukumu yao ili shughuli za kawaida zisiathirike.
Bw Ruku alisema washukiwa wanatarajiwa kukamatwa kabla ya muda huo kukamilika, akitaja hasa maafisa wa Idara ya Magereza.
Uchunguzi wa awali umebaini dosari za kutia shaka katika rekodi za ajira. Baadhi ya wafanyakazi wana rekodi zinazoonyesha waliajiriwa kabla ya kuzaliwa, huku wengine wakionekana kuanza kazi kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Pia, kuna visa vya wafanyakazi wengi kutumia akaunti moja ya benki kupokea mishahara.
Serikali inatarajia kuwa zoezi hilo litasaidia kubaini dosari katika mfumo wa malipo, kuwachukulia hatua wanaohusika na kulinda fedha za umma dhidi ya matumizi mabaya.