Habari

Samia ndiye rais, apata asilimia 98 ya kura

Na CHARLES WASONGA Na REUTERS November 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS Samia Suluhu Hassan ametangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais Tanzania huku fujo zikishuhudiwa nchini humo tangu siku ya uchaguzi Jumatano.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (NIEC) Samia alipata asilimia 98 ya kura zilizopigwa, sawa na karibu kura milioni 32.

Hii ina maana kuwa ataapishwa na kuanza kuongozwa kwa muhula mkamilifu kama Rais wa Tanzania. Mama Samia aliingia mamlakani mnamo Machi 21, 2021 kufuatia kifo cha marehemu John Pombe Magufuli.

“Namtangaza Samia Suluhu Hassan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama mshindi katika uchaguzi wa urais,” akasema Jacob Mwambegele, mwenyekiti wa NIEC, Jumamosi, Novemba 1, 2025, akitangaza matokeo hayo.

Katika kisiwa cha Zanzibar (ambacho ni sehemu ya Tanzania), kinachochagua kiongozi wake na serikali, Rais Hussein Mwinyi wa chama cha CCM alishinda kwa kupata asilimia 80 ya kura.

Viongozi wa upinzani kisiwani humo walilalamika kuwa uchaguzi huo ulisheheni visa vingi vya udanganyifu.

Waangalizi wa kimataifa wamelalamikia utovu wa uwazi na ghasia zilizoripotiwa wakati wa uchaguzi Tanzania ambapo imeripotiwa kuwa mamia ya watu walikufa na wengine wakajeruhiwa.

Imekuwa vigumu kubaini idadi kamili ya watu waliokufa kwani serikali ya Tanzania ilizima intaneti na kutangaza amri ya kutotoka nje ili kuzima machafuko.

Maandamano yalishuhudiwa katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha miongoni mwa mingine. Waandamanaji waliharibu mabango yenye picha za Samia huku wakishambulia vituo vya kupigia kura na vituo vya polisi.

Hii ni licha ya onyo kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Tanzania na hatua ya maafisa wake kujitokea barabara kujaribu kutuliza hali.

Waandamanaji hao, wengi wao wakiwa vijana, wamepuuzilia mbali uchaguzi huo wakisema haukuendeshwa kwa njia ya haki.

Waliisuta serikali ya Rais Samia kwa kuhujumu demokrasia kwa kuwazima viongozi wakuu wa upinzani kushiriki uchaguzi huo.

Wao ni Tundu Lissu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Luhaha Mpina wa chama cha ACT-Wazalendo.

Bw Lissu anazuiliwa gerezani kwa kosa la uhaini.

Inasemekana kuwa mnamo Aprili mwaka huu aliwachochea raia wa Tanzania kususia uchaguzi mkuu hadi serikali itakapotekeleza mageuzi katika mfumo wa uchaguzi.