Saraha Wairimu mjane wa Cohen amteua wakili Pravin Bowry kumtetea
SARAH Wairimu, mjane wa Tob Cohen anayekabiliwa na mashtaka ya kumuua mumewe miaka sita iliyopita amemteua wakili mwenye tajriba ya juu Pravin Bowry kumtetea kwenye kesi hiyo.
Alipofika mbele ya Jaji Diana Kavedza , Bw Bowry aliomba asome faili ya kesi hiyo dhidi ya Sarah kabla ya kuteuliwa siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo.
Jaji Kavedza alimkubalia Bw Bowry kusoma ushahidi katika kesi hiyo na kuamuru kesi hiyo itajwe Novemba 27,2025 kwa maagizo zaidi.
Sarah amekana shtaka la kumuua mumewe 2019.
Na wakati huo huo Sarah alishhtakiwa upya kutoa habari uwongo kwa polisi kuhusu pasipoti yake.
Sarah alishtakiwa mnamo Novemba 7 2025mbele ya hakimu mkuu Zainab Abdul kwa kudanganya mkuu wa kituo cha polisi cha Munyange eneo la Othaya kaunti ya Nyeri Inspekta Mercy Riungu kwamba alipoteza pasipoti yake.
Kufuatia ripoti hiyo ya Feburuari 20 2023 Insp Riungu alimpa Sarah abstrakti ya kumwezesha kupata pasipoti nyingine.
Shtaka lilisema Sarah alimdanganya Insp Riungu pasipoti yake nambari BK043532 ilipotea.
Shtaka la pili lilisema kuwa mnamo siku hiyo Feburuari 20 2023, Sarah alienda kwa wakili Muchiri WaGathoni na kuapa uwongo kwamba pasipoti yake imepotea.
Sarah alikana mashtaka yote mawili kisha akaomba aachiliwe kwa dhamana.
Upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo la dhamana na kufafanua kwamba Sarah anakabiliwa na mashtaka ya kumuua Tob Cohen na amenyimwa dhamana na Jaji Diana Kavedza.
Sarah ameshtakiwa kumuua mumewe Tob Cohen mnamo Julai 19 2019 katika makazi yao eneo la Lower Kabete.
Mwili wa Cohen ulikutwa umetupwa ndani ya shimo la choo ukiwa umefungwa kwa blanketi.
Hakimu mkuu Zainab Abdul alitupilia mbali ombi la dhamana la Sarah akisema “hastahili kuachiliwa kwa dhamana.”
Bi Abdul alisema mahakama kuu ilinyima mshtakiwa dhamana kwa vile yuko na pasipoti mbili.
Pia alisema mahakama kuu ilimnyima dhamana kwa madai aliwatisha mashahidi.
Jaji Kavedza amemnyima dhamana mara mbili.
Sarah kupitia wakili wake wa hapo awali amekata rufaa kupinga uamuzi Jaji Kavedza kumnyima dhamana.
“Utasalia ndani hadi mahakama ya rufaa iamue hatma yako ya dhamana. Ikiwa utaachiliwa na mahakama ya rufaa basi utawasilisha upya ombi lako la dhamana,” Bi Abdul alimweleza mshtakiwa.
Pia aliamuru Sarah aendelee kuzuiliwa katika gereza la wanawake ya Langata.
Mwili wa Cohen ilikutwa imetupwa ndani ya shimo la choo ikiwa imefungwa kwa blanketi.