Sauti mtaani kuhusu madai ya uhai wa Ruto kuwa hatarini
Na MWANGI MUIRURI
BW Michael Kariuki: “Madai kuwa uhai wa Naibu Rais William Ruto uko hatarini ni siasa.”
Kamlesh Kamau: “DP Ruto ndiye mlalamishi na anafaa kuandikisha taarifa ndio ukweli halisi ujitokeze.”
Eneo la Mlima Kenya kwa sasa linajadili hoja moto ya ikiwa kuna ukweli wowote kuwa kuna anayetaka kumuangamiza Naibu Rais, Dkt William Ruto.
Mnamo Jumatatu na kufikia Jumanne, mjadala huo umeshika kasi baada ya kitengo cha uchunguzi wa Jinai (DCI) kuwapa mwaliko mawaziri wanne wakaandikishe taarifa kuhusu ‘njama’ hiyo.
Waliodaiwa kuwa katika njama hiyo ni mawaziri Sicily Kariuki (Afya), James Macharia (Wizara ya Uchukuzi), Peter Munya (Biashara na Viwanda) na Joe Mucheru wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Pamoja nao, wanadaiwa kuwa makatibu maalumu na pia wakurugenzi wa mashirika ya kiserikali, cha maana kusisitiza ikiwa ni kwamba, washukiwa hao wote ni wa Mlima Kenya.
Ni madai ambayo yamezua hasira ya wale ambao hupinga azima ya DP Ruto ya kurithi ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, wakisuta madai hayo kama yasiyo na mashiko na nia ya kuaibisha serikali, kugawanya baraza la mawaziri na kuwaharibia sifa waliotajwa.
Kwa wale ambao humuunga mkono DP Ruto katika siasa hizo za urithi wamesisistiza kuwa ni lazima madai hayo yachunguzwe kwa kina na wote ambao watakuwa katika hatia ya kupanga njama kama hiyo waadhibiwe kwa mujibu wa kisheria.
Kama kawaida, wakati masuala moto ya kisiasa yamezuka, huwavutia wote kuchangia, walio na ufahamu, wasio nao na wa kuchangia tu ndio wajipate sauti yao imesikika, hata ikiwa hakutakuwa na umakinifu wowote wa kimawazo kuhusu suala hilo.
“Mimi kile ninajua ni kwamba hakuna ukweli wowote kuhusu madai hayo bali ni siasa zinachezwa. Mtu aliye na hadhi ya Naibu Rais ataanza kulialia namna gani kuwa wadogo wake wanataka kumuua? Si angeamrisha kikosi cha polisi kuwaandama kwa uhakika washukiwa hao kwa nguvu zote za kiserikali?” ahoji Bw Michael Kariuki, mwenyeji wa Kaunti ya Nyeri.
Kwa upande wake, Kamlesh Kamau kutoka Kaunti ya Murang’a anasema hizi siasa zina “utoto fulani sasa.”
“Hili sio suala la kuangazia katika jukwaa la umma. Ni suala la kiserikali kwa kuwa ni maafisa ndani ya serikali moja ambao wanadaiwa kuwa katika njama sawa na ya kimapinduzi,” anasema Kamau.
Anasema kuwa suala la kupanga njama ya kuua Naibu Rais ni la kuogofya.
“Sitaki kuwazia kuhusu ni hali gani inaweza ikazuka ikiwa kuna ukweli wowote ndani ya madai haya. Ruto ndiye anaweza kutupa ukweli halisi kuhusu suala hili kupitia kujitolea kwake kusaidia Wakenya kulielewa. Ruto alalamike rasmi na apeane ushahidi alio nao kwa kuwa yeye ndiye mlalamishi. Maafisa wa kiusalama wachunguze na kisha taifa lipewe jibu la uhakika. Lakini katika hali ya sasa, tutapiga domo, mitandaoni kuwekwe majibu ya upuzi, vyombo vya habari vibashiri na kujaribu uchambuzi usiotufaa na suala hili lote ligeuke kuwa kelele,” anasema Kamau.
Anasema kuwa ni jukumu la Ruto kusaidia kuanika washukiwa hao ikiwa kwa kweli ni wakatili kiasi hicho.