Sekta ya utalii yaonekana kufufuka, wageni waongezeka kwa asilimia 60
SEKTA ya utalii inaonekana kufufuka baada ya kuandikisha ongezeko la kima cha asilimia 60 la watalii wanawasili nchini tangu 2022, kulingana na takwimu kutoka kwa Wizara ya Utalii.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa watalii 2.4 milioni walitembelea Kenya mnamo 2024, ikilinganishwa na watalii 1.5 milioni waliowasili 2022.
Akizungumzia takwimu hizo kutoka kwa wizara yake, Waziri wa Utalii Rebecca Miano alisema ongezeko hilo la idadi ya watalii limewezesha mapato kutoka kwa sekta hiyo kupanda hadi Sh452 bilioni, kutoka Sh268 bilioni miaka miwili iliyopita.
“Kwa muda mrefu watalii wamekuwa wakizuru fuo na mbuga za wanyama pekee licha ya uwepo wa vivutio vingine vya watalii kote nchini. Kwa mfano watalii wanaweza kuzuru maeneo ya kispoti, kitamaduni, kilimo na kiafya,” Bi Miano akasema.
Alieleza kuwa ongezeko la idadi ya watalii wanaozuru nchini limechangia Sh509 bilioni kwa utajiri wa nchini, ambao ni asilimia 2.6 ya mchango wa sekta hiyo unaokadiriwa kuwa ya thamani ya Sh1 trilioni.
Vile vile, data zinaonyesha kuwa idadi ya wanaoajiriwa imepanda katika sekta hiyo, huku ikikadiriwa kuzalisha nafasi 1.5 milioni 2024 kutoka nafasi 1.1 milioni mnamo 2022.
Waziri Miano alisema katika juhudi za kupunguza utegemezi kwa watalii wanaozuru fuo na mbuga za wanyama, wizara yake imekuwa ikipanua maeneo mapya ya kuvutia watalii.
Aidha, alitambua kwamba shughuli za michezo kama vile mashindano ya Magical Kenya Open, Kip Keino Classic na mbio za magari za Naivasha WRC Rally zimeondokea kuvutia idadi kubwa ya watalii.
“Hafla za kitamaduni kama Tamasha ya Jamii za Maa na Tamasha ya Rusinga pia zinaendelea kuwa vituo kwa watalii,” Bi Miano akaeleza.
Isitoshe, utalii wa makongamano umevutia katika miaka ya hivi karibuni ambapo Kenya ilikuwa mwenyeji wa mikutano, makongamano na maonyesha 643, 595 yaliyovutia idadi kubwa ya wageni kutoka mataifa ya kigeni mnamo 2024. Idadi hii inawakilisha ongezeko la asilimia 12.5 ikilinganishwa na mwaka wa 2022.
Wizara ya Utalii pia imekuwa ikivumisha utalii wa humu nchini, hasa baada ya janga la Covid-19 lililoshuhudiwa kati ya miaka ya 2020 na 2021.
Inafanya hivyo kupitia kampeni kama vile “Tembea Kenya” inayohusisha kupunguzwa kwa ada ya kuingia mbuga za wanyamapori na kupunguzwa kwa ada za usafiri kwa watu wa familia moja.
Kampeni hizo zimechangia idadi ya watalii wa humu nchini wanaokodisha wanalala kwenye mikahawa kupanda hadi zaidi ya 5.1 milioni mnamo 2024.