Habari

Seneti kuamua hatima ya mchakato wa kufanya Thika kuwa jiji la 6 Kenya

Na COLLINS OMULO July 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MASENETA ndio wanashikilia ndoto ya serikali ya Kaunti ya Kiambu kupandisha Thika kuwa jiji la sita nchini Kenya.

Hii inafuatia hatua ya mchakato wa kupandisha hadhi Manispaa ya Thika kuwasilishwa rasmi katika Seneti, ambapo Kamati ya Ugatuzi sasa inashughulikia uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Kiambu lililopitisha ombi hilo.

Mwezi uliopita, madiwani wa Kiambu waliidhinisha kupandishwa kwa Thika kuwa jiji, wakizingatia mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Mipango Miji na Maendeleo ya Miji ya bunge hilo.

Jumanne, Spika wa Seneti Amason Kingi alielekeza kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Wajir, Mohamed Abass, kuharakisha kuchunguza na kuwasilisha ripoti kuhusu uamuzi huo wa kaunti ya Kiambu.

“Ninaagiza kamati kushughulikia suala hili kwa haraka na kuwasilisha ripoti kwa mjadala na uamuzi wa Seneti,” alisema Spika Kingi.

Macho yote sasa yameelekezwa kwa kamati hiyo kuona iwapo itakubaliana na uamuzi wa Bunge la Kaunti.

Iwapo Seneti itapitisha mapendekezo hayo, Karani wa Seneti atawasilisha kwa Rais William Ruto ili kutoa Hati rasmi ya kupandisha Thika kuwa jiji.

Kwa sasa, kuna majiji matano nchini: Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Eldoret.Gavana wa Kiambu, Kimani Wamatangi, aliyeongoza ujumbe kutoka serikali ya kaunti na bunge la kaunti hadi Seneti wakati wa kuwasilisha azimio hilo, alielezea matumaini kuwa Seneti itaidhinisha pendekezo hilo.