Habari

Serikali kufanikisha UHC kupitia ufadhili na huduma bora

Na CECIL ODONGO October 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI sasa imetangaza mpango ambapo inalenga kuoanisha mahitaji ya afya pamoja na yale ya kifedha kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata huduma bora za afya.

Katibu katika Wizara ya Afya anayesimamia huduma za matibabu Dkt Ouma Oluga na mwenzake wa Wizara ya Fedha Chris Kiptoo wamesema lengo kuu ni kuhakikisha kwamba Wakenya wananufaikia kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC).

Wawili hao Alhamisi waliandaa mkutano wa kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mpango wa UHC unaoana na ule wa mfumo wa kiuchumi wa kuwainua wananchi wa mapato madogo.

Dkt Oluga alitaja kuimarisha kwa hospitali za kiwango cha rufaa, matumizi ya teknolojia katika kufanikisha huduma za kimatibabu, utafiti, uvumbuzi wa kimatibabu na pia utengenezaji wa chanjo, kama masuala ambayo serikali inalenga kuhakikisha yanafanikishwa.

Aliongeza kuwa huduma bora za afya zitafanikiwa tu iwapo mgao unaotengewa sekta hiyo utatosha na pia utawasilishwa kwa wakati.

“Bajeti finyu na pia ukosefu wa ufadhili unaathiri utoaji huduma kwenye hospitali za rufaa, asasi za utafiti na pia mipango ya afya ya kijamii,” akasema Dkt Oluga.

Naye Bw Kiptoo alisema kuwa kupitia ufadhili wa kutosha, serikali inalenga kufanikishwa kwa utekelezaji wa UHC na pia kushusha gharama ya matibabu kwa kila Mkenya.

Makatibu hao wawili waliahidi kuhakikisha kuwa mfumo upo ambapo fedha zitakuwa zikitolewa kwa wakati kugharimia huduma za afya. Hili litachangia kutokwepo kwa pengo ambalo linasababisha ukosefu wa huduma kwa Wakenya.

Aidha, makatibu hao wawili walisisitizia kwamba hoja za kimsingi katika kufanikisha UHC ni mageuzi katika ufadhili wa sekta ya afya, mageuzi ya kidijitali, uwekezaji katika sekta ya afya na kurahisishwa kwa upatikanaji wa huduma za afya kwa Wakenya wote.

Mnamo Aprili mwaka huu, Waziri wa Afya Aden Duale, alitangaza kwamba Wakenya milioni 21.3 wanapata huduma bora za afya chini ya mpango wa UHC.