Habari

Serikali mbioni kubuni tume kukiendeleza Kiswahili nchini

February 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

SERIKALI iko mbioni kubuni Tume ya Kitaifa ya Kiswahili ambayo itahusika katika uendelezaji wa Kiswahili nchini, kama mojawapo ya nguzo kuu zinazowaunganisha Wakenya.

Kulingana na Katibu katika Wizara ya Utamaduni na Turathi za Kitaifa, Bi Josephta Mukobe, tume hiyo pia itawianisha mikakati ya ukuzaji wa Kiswahili nchini.

Akihutubu Alhamisi jioni, katika hafla ya Tuzo ya Fasihi ya Mabati-Cornell jijini Nairobi, Bi Mukobe alisema kuwa tayari wizara hiyo imekusanya maoni ya wananchi katika maeneo mbalimbali; ambayo yatatumiwa baadaye kwenye harakati za kubuni tume hiyo.

“Tushazunguka katika sehemu tofauti nchini na kupokea maoni ya wananchi kuhusu mambo ambayo wangependa yajumuishwe kwenye harakati za uundaji wa tume hiyo,” akasema Bi Mukobe.

Kauli yake inajiri huku serikali ikionekana kujivuta kwenye harakati za kukikweza Kiswahili kama lugha rasmi nchini, licha ya kupata utambuzi huo kwenye Katiba.

Kenya pia imekosolewa pakubwa na wadau mbalimbali kwa kukosa kuchukua hatua za kutosha kuikuza lugha hiyo, licha ya kushiriki kwenye harakati zingine za kikanda, kama kubuniwa kwa Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC).

Wadau nchini pia wamekosolewa kwa kutoonyesha umoja, kwenye juhudi za kuikuza na kuendeleza lugha hiyo.

Hata hivyo, Bi Mukobe alisema kuwa Wakenya wenyewe ndio wana jukumu la msingi kuendeleza lugha hiyo, akiwakosoa kwa mazoea ya matumizi ya Kiingereza katika majukwaa mbalimbali.

“Ni sikitiko kuwa hadi sasa, Kiswahili bado kinachukuliwa kama lugha ya watu ambao hawajasoma. Hili ni tatizo letu wenyewe, ambalo lazima tulibadilishe, hasa katika maeneo rasmi kama afisi,” akasema.

Kwenye mashindano hayo, waandishi kutoka Tanzania waliwapiku wenzao kutoka Kenya, wakiibuka washindi kwenye vitengo vya riwaya na ushairi.

Katika kitengo cha riwaya, mwandishi Lello Mmassy kutoka Tanzania aliibuka mshindi kwa riwaya yake ‘Mimi na Rais’.

Mwandishi chipukizi Wanyoni John Wanyama kutoka Kenya aliibuka wa pili kwa riwaya yake ‘Safari ya Matumaini’ huku mwandishi Theuri Maina akishiklia nafasi ya tatu kwa riwaya ‘Ziaka Imetoboka’.

Watanzania walitawala katika kitengo cha Ushairi, kwani washindi wote wanatoka nchini humo.

Mwandishi Moh’d Khamis Songoro aliibuka mshindi kwa diwani ‘Nusu ya Moyo’, akifuatiwa na Bw Arshad Ali kwa diwani ‘Mji wa Kambare!’ Diwani ya Mnenaji!’, huku Nassor Hilal Kharusi akiibuka wa tatu kwa diwani ‘Mama Usihuzunike’.

Kharusi ni mzaliwa wa Zanzibar, ingawa anasomea Tanzania bara.

Washindi katika vitengo vyote walituzwa Sh500,000 huku mshindi wa pili akituzwa Sh250,000.

Wazungumzaji mbalimbali walisisitiza kuhusu haja ya mashirika mbalimbali na watu wenye uwezo kuunga mkono juhudi za kukuza lugha za Kiafrika.

Shindano hilo lilianzishwa mnamo 2014 na Prof Mukoma wa Ngugi – mwanawe mwandishi maarufu Ngugi wa Thiong’o – na Bi Elizabeth Attree.

Mwenyekiti wa bodi ya Tuzo ya Mabati-Cornell Mwalimu Abdilatif Abdalla ahutubu Februari 27, 2020, katika hoteli ya Intercontinental, Nairobi. Picha/ Hisani

Hufadhiliwa na Chuo Kikuu cha Cornell kutoka Amerika na kampuni ya kutengeneza mabati ya Mabati Rolling Mills.

Mwaka huu, Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o ulikuwa miogoni mwa wafadhili wakuu.

Jumla ya Sh6 milioni zimetolewa kwa washindi tangu kuanzishwa kwake.

Miongoni mwa wale waliohudhuria ni mbunge wa Kamukunji Bw Yusuf Hassan na Katibu katika Wizara ya Utalii Bi Safina Kwekwe.