Serikali tuliyochagua imeamua kutuua, walia wakazi wa Angata Barikoi simanzi ikitanda
SIMANZI, majonzi na hasira zimetanda katika vijiji vya Angata Barikoi, Kabusa, na Tendwet, katika eneo la Trans Mara, Kaunti ya Narok, baada ya polisi kuua watu sita, wakiwemo vijana wadogo waliokuwa wanafunzi na wakazi wasiohusika na mzozo wa ardhi.
Vurugu hizo zililipuka Jumatatu baada ya wakazi kupinga jaribio la kugawa kwa nguvu ardhi yenye ukubwa wa ekari 6,800 katika eneo la Moyoi, iliyoongozwa na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo (DCC), Bw Abdihakim Jubat, kwa usaidizi wa maafisa wa ardhi na polisi wa GSU.
Katika hali ya kushangaza na ya kutisha, watoto na vijana waliokuwa wakishuhudia tukio hilo waliuawa kwa kupigwa risasi.
Katika kijiji cha Kipsindenet, Bw John Kirui aliangua kilio akisimulia kuuawa kwa mwanawe wa kwanza, Gideon Kipkorir Koech, mwanafunzi wa Sekondari ya Ngendalel mwenye umri wa miaka 15.
“Mwanangu alikimbia kuangalia kilichokuwa kikiendelea. Polisi walikuwa wakifyatua risasi kwa yeyote aliyeonekana. Risasi ilimpiga kichwani. Nimeumia mno. Serikali ya Ruto ni kama janga kwa wananchi,” alisema kwa uchungu.
Mamake marehemu, Bi Nancy Kirui, aliongeza kuwa alikuwa akimtegemea sana kijana huyo, hasa wakati mumewe alikuwa safarini kutafuta riziki.
Katika kijiji cha Kabusa, familia ya aliyekuwa naibu chifu, Bw Paul Ng’eno, inaomboleza kifo cha mwanao Isaiah Koech Ng’etich, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Eldoret aliyepaswa kuhitimu mwaka 2026.
Alipigwa risasi kifuani.
“Hakuhusika kabisa na ardhi hiyo inayozozaniwa. Viongozi walioletwa na polisi walishindwa kuhakikisha amani. Huu ni msiba mzito,” alisema baba yake.
Mjomba wake, Bw Stephen Lang’at, alielezea hasira yake kwa serikali ya Rais Ruto, akisema: “Serikali hii tunayopigia kura imeamua kutuua. Rais Ruto anaongoza watu wanaouawa, maskini na walemavu. Je, ataongoza nani? Hata marais waliopita hawakutuua!”
“Tunataka Rais William Ruto atafakari dhuluma ambayo serikali yake imeitendea familia yetu. Je, ataweza kweli kuongoza watu waliokatwa viungo, walioporwa kila kitu au waliouawa?” alihoji Bw Lang’at.
Alishangaa jinsi serikali inaweza kuamua kuwaua wananchi wake inayopasa kuwalinda kikatiba.
“Bw Ruto, wewe ni Rais wa tano wa Kenya. Wametangulia wengine lakini hakuna aliyewahi kuwaua watu wetu. Tumechoshwa na serikali yako. Hata mtu yeyote aliyevaa sare ya serikali anatukera sasa,” alisema kwa ukali.
Katika kijiji cha Tendwet, Bi Janet Parsupen bado hajakubali kuwa mjane baada ya mumewe, Paul Parsupen, mwenye umri wa miaka 48, kuuawa kwa risasi na polisi.
“Ninaumia mno. Naomba mume wangu apate haki,” alisema kwa uchungu.
Mbunge wa Kilgoris, Bw Julius Sunkuli, alipotembelea familia zilizoathirika, alilaumu serikali kwa kuchochea ghasia hizo.
“DCC aliambiwa hali si salama lakini akaamua kuendelea. Sasa tunaomboleza vifo vya watu sita. Serikali lazima iwajibike,” alisema.
Jumanne, Mkuu wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai Mohammed Amin, waliongoza kikao cha usalama eneo hilo na kuagiza kuhamishwa mara moja kwa Bw Jubat na DCIO wa Lolgorian, Bw Too.