Habari

Serikali yaelekea kupoteza Sh100 milioni kwenye ununuzi tata wa ardhi ya wakimbizi

Na ERIC MATARA July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HUENDA serikali ilipoteza zaidi ya Sh100 milioni kwenye ununuzi tata wa shamba ili kuwapa makao wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Haya yamefichuka baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Nakuru kurejesha cheti cha umiliki ardhi kwa wamiliki wake asili. Hii ni baada ya baadhi ya wanafamilia kupinga kuuzwa kwa mashamba yao ya tangu jadi.

Makubaliano haya yaliishia serikali kununua ekari 755 ya ardhi kwa wamiliki wa Shamba la Ndonga, eneo la Subukia, Kaunti ya Nakuru.

Wahanga 266 wa ghasia za uchaguzi mkuu walipewa ardhi hiyo.

“Mahakama inaamrisha serikali ilitoe hati ya umiliki wa ardhi ya ekari 755 kwa familia. Wakimbizi nao wanazuiwa kugawanya shamba hilo linalofahamika kama Ndonga ambalo liliuzwa kwa njia haramu kuwapa makao,” akasema Jaji Heston Nyaga.

Mahakama ilimwaamrisha Waziri wa Ardhi Alice Wahome binafsi awasilishe cheti hicho cha umiliki ardhi kortini ili kiwasilishwe kwa familia.

Uamuzi huo wa mahakama ni pigo kwa wakimbizi ambao walikuwa wametengewa ploti katika shamba hilo. Korti pia iliwazuia kujenga na kuishi katika shamba lenyewe.

Pia ilibainika kuwa stakabadhi zilizotumika kuuza ardhi hiyo kati ya Wizara ya Mipango Maalum na wauzaji, zilikuwa zimeghushiwa.

Katika kesi hiyo, Irene Kanyi, Mary Nyambura, Wangechi Mburu, Winnie Muthoni, Hellen Mureithi, Zipporah Waringa, Harriet Wanjiru, Loise Wanjiku, Mary Wangari na Penina Wangui walidai ndugu yao Philip Kamau Njoroge alitumia stakabadhi zilizokuwa zimeghushiwa kufanikisha mauzo hayo.

Familia hiyo ilishtaki Mwanasheria Mkuu, Katibu katika Wizara ya Ardhi na mwenzake aliyehudumu chini ya wizara ya Mipango Maalum. Wakimbizi hao walijiunga katika kesi hiyo kama washirika.

Kwa mujibu wa wakili wa familia, stakabadhi ambazo zilitumika kwenye mauzo ya shamba hilo zilikuwa zimeghushiwa na saini hazikuwa za wanafamilia wengine ambao walisajiliwa kama wamiliki wa ardhi hiyo.