Serikali yajengea babake Albert nyumba mpya, yaweka pia stima
GAVANA wa Homa Bay Gladys Wanga ametimiza maono ya Albert Ojwang ya kujengea wazazi wake nyumba mpya ya kisasa.
Serikali ilifadhili ujenzi wa nyumba hiyo ya vyumba viwili vya kulala ya Mechack Opiyo na mkewe Eucabeth Adhiambo katika kijiji cha Kakoth, lokesheni ya Kokwanyo.
Ujenzi wa nyumba hiyo ulianza Juni 16 wakati mkuu huyo wa kaunti na mbunge wa Kabondo Kasipul Eve Obara walitembelea boma na kuweka jiwe la msingi.
Siku hiyo hiyo, Bi Wanga na mbunge huyo walitoa fedha ambazo zilitumwa na Rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga.
Jumla ya Sh3 milioni zilipewa Bw Opiyo huku Rais akitoa Sh2 milioni.
Ni hapo ambapo Gavana Wanga alitangaza kwamba atasaidia familia kupata nyumba mpya kuafikia matamanio ya Ojwang.
“Albert alifariki wakati ambapo alikuwa anapanga kusaidia wazazi wake kwa kuwajengea makao mazuri. Nitahakikisha hili linafanyika,” alisema wakati wa ziara hiyo.
Siku 16 baadaye, nyumba hiyo iko tayari kuhamiwa.
Bw Opiyo na mkewe walikuwa wakiishi katika nyumba ambayo haikuwa katika hali nzuri.
Makazi yote sasa yamebadilika baada ya Wakenya wenye moyo wa kusaidia akiwemo Gavana Wanga kubadilisha hali.
Nyumba hiyo imebadilisha kabisa mandhari ya makazi hayo.
Ile nyumba nzee imebomolewa.
Bw Opiyo na mkewe wanatarajiwa kuhamia nyumba hiyo mpya Alhamisi wakati mwili utapelekwa kutazamwa kabla ya mazishi siku inayofuata.
Nyumba hiyo ina paa nzuri pamoja na sakafu ya vigae.
Tanki la maji pia limewekwa pamoja na viti vipya.
“Kila kitu kwenye nyumba ni kipya ikiwemo viti na malazi. Tumehakikisha pia kwamba imewekwa stima,” akasema Bi Wanga.