Habari

Serikali yapambana kuokoa Margaret Nduta dhidi ya hukumu ya kifo Vietnam

Na CECIL ODONGO March 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KATIBU katika Wizara ya Masuala ya Nje Korir Sing’oei Jumapili aliandaa mazungumzo ya simu na mwenzake wa Vietnam kuhusiana na juhudi za kumwokoa Mkenya Margaret Nduta anayekabiliwa na hukumu ya kitanzi nchini humo.

Bw Singóei alisema Naibu Waziri wa Masuala ya Kigeni Nguyen Minh Hang alimhakikishia kuwa  ombi la Kenya kuwa Nduta asinyongwe lilikuwa likitathmniwa.

“Nilimwambia Bi  Hang kuhusu wasiwasi wa Wakenya kuhusiana na  kitanzi kilichokuwa kikinukia kwa raia wetu na kuomba hukumu hiyo isitekelezwe. Hiyo itatoa muda kwa Kenya na Vietnam kusaka muafaka ya kupata suluhu kwa suala hili,” akasema Bw Singóei kupitia ukurasa wake wa X.

Naibu Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Vietnam Nguyen Minh Hang (kushoto) alipokutana na Katibu wa Mashauri ya Kigeni Korir Sing’oei. Picha|Hisani

“Nashukuru sana kwamba Bi Hang alinihakikishia kuwa ombi letu linatathminiwa na utawala wa Vietnam,” akaongeza.

Katibu huyo aliwahakikishia Wakenya kuwa ubalozi wa nchi kule Vietnam ulikuwa ukifuatilia kesi hiyo kwa lengo la kuhakikisha Nduta hakutani na kamba.

Baada ya kilio kutoka kwa Wakenya kuhusiana na masaibu ya Nduta, serikali ilionekana kuchukua hatua za kidiplomasia kuokoa raia wake Jumapili.

Kesi ya Nduta ina vizingiti vingi na ni ngumu lakini tunafanya kila kitu tuwezalo kuhakikisha tunamnusuru,

Alikuwa akirejelea barua ambayo Seneta wa Kisii Richard Onyonka aliandika kumwomba Rais William Ruto aingilie kati ili kumwokoa Nduta aliyekuwa amesalia na muda mchache tu kabla ya kunyongwa.

Katika barua hiyo ya Machi 14, Bw Onyonka alimtaka Rais azungumze na utawala wa Vietnam ili Mkenya huyo arejeshwe nchini.

Nduta, 37 alihukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya na ameratibiwa kunyongwa Jumatatu.

Pia Bw Onyonka alimtaka Rais ashirikishe Umoja wa Mataifa, makundi ya kimataifa ya haki ili Nduta apewe adhabu nyingine au arejeshwe Kenya.