Serikali yapuuza madai ya Ruto kuhusu kura 2022
NAHASHON MUSUNGU na ONYANGO K’ONYANGO
KATIBU wa Wizara ya Usalama wa Nchi, Dkt Karanja Kibicho, amepuuzilia mbali madai ya Naibu Rais William Ruto kuhusu uwepo wa watu wenye ushawishi serikalini wanaopanga kuvuruga azma yake kuwania urais 2022.
Bila kutaja jina, Dkt Kibicho pia alisema huenda Dkt Ruto anaogopa kushindwa kwenye uchaguzi huo.
Alisema hayo Jumatano kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.
“Watu hao hawapo. Serikali imebuniwa kwa mpangilio ambapo tunaweza kufuatilia chochote kinachoendelea.
Unajua kuna watu wengi ambao huwa tunawasikia na pia tunashangaa wao ni nani. Wakati watu hawakuelewi, jaribu kuwafafanulia,” akasema.
Katibu huyu alizungumza siku moja baada ya Dkt Ruto kudai kwamba watu fulani serikalini wanapanga kusambaratisha mpango wake kuwania urais kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.
Alisema njama hizo ni pamoja na kumwibia kura. Hata hivyo, alisema yuko tayari kwa makabiliano.
“Watu wanasema kuwa kuna ‘system’, eti kuna watu watatuibia kura. Eti kuna watu watafanya maamuzi hata wananchi wakipiga kura. Nataka kusema ninawangoja. Nitakuwa na wananchi na Mungu,” akasema Jumanne alipowahutubia viongozi na ujumbe kutoka Kaunti ya Kajiado waliomtembelea kwenye makazi yake katika mtaa wa Karen, jijini Nairobi.
Mbali na Dkt Ruto, kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi na Dkt Oburu Odinga wameeleza kuhusu uwepo wa watu hao serikalini katika nyakati tofauti.
Viongozi wanaoegemea upande wa Dkt Ruto walisisitiza kuwa wanategemea wananchi wala si watu wenye ushawishi kuunda serikali ijayo.
Vikao
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee (JP) Caleb Kositany alisema Dkt Ruto anawategemea wananchi na ndiyo sababu ameamua kufanya vikao vinavyowahusisha moja kwa moja badala ya kukutana na wanasiasa kwenye majumba ya kifahari.
“Kwa upande wetu, hatuogopi vitisho vya watu hao. Wapinzani wetu wanatuogopa. Badala ya kuwafikia wapigakura, wanangojea kuungwa mkono. Kwa mfano, mnamo 2002, marehemu Daniel Moi alitangaza kumuunga mkono Rais Kenyatta lakini mpango huo haukufaulu kwani Wakenya walikuwa washaamua kwamba wanataka mabadiliko. Hilo ndilo litafanyika 2022,” akasema Bw Kositany, ambaye pia ndiye mbunge wa Soy.
Wabunge Nelson Koech (Belgut) na Didmus Barasa (Kimilili) wamekuwa wakiongoza mikutano ya kumpigia debe Dkt Ruto katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kama washirika wa Dkt Ruto, tumeamua kuanza vikao kukutana na wananchi mashinani kinyume na wenzetu wanaoendelea kufanya vikao katika majumba ya kifahari na kubuni mikataba ya kisiasa Nairobi na Kajiado. Sisi tutaendelea kuwafikia wananchi popote walipo. Matunda ya juhudi zetu yameanza kudhihirika,” akasema.
Kundi hilo limeamua kuendesha dhana ya ‘Maskini dhidi ya Matajiri’ linaloamini itakumbatiwa na Wakenya, hasa vijana.
Huku washirika wake wakiendelea kumpigia debe katika maeneobunge yao, Dkt Ruto amekuwa akikutana na jumbe kutoka sehemu mbalimbali nchini kwenye makazi yake.