SGR imefanya uchumi kudorora Pwani – utafiti
NA ANTHONY KITIMO
HALI ya uchumi Pwani inazidi kudorora huku serikali kuu ikikosa kupata zaidi ya Sh126 bilioni kutokana na athari za amri ya serikali kusafirisha mizigo yote kwa kutumia reli ya kisasa ya SGR, utafiti umebaini.
Katika ripoti iliyotolewa Ijumaa na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) na kukabidhiwa Gavana wa Mombasa na viongozi wengine kutoka Pwani, ilionyesha kuwa asilimia 60 ya watu waliokuwa wakifanya kazi katika mabohari ya mizigo (CFS) wamefutwa kazi huku madereva wa matrela wakiathirika kwa kiasi kikubwa.
Naibu Chansela wa chuo kikuu cha Nairobi Profesas Julius Ogeng’o ambaye aliongoza kundi la watafiti alisema uchumi hasa katika kaunti wa Mombasa umedorora kwa kiasi kikubwa kwa muda wa mwaka mmoja uliopita.
Takwimu zilionyesha kuwa wafanyikazi 2,987 katika sekta mbalimbali zikiwemo CFS, maajenti wa kukagua mizigo na wanaofanyakazi katika maduka ya vipuri, wamepoteza kazi kwa muda wa mwaka mmoja uliopita huku wafanyikazi zaidi wakitarajiwa kukosa kazi iwapo amri hiyo haitasitishwa.
“Leo tumekutana na viongozi wa Pwani wakiongozwa na Gavana Joho na kuwasilisha ripoti yetu lakini inadhihirisha kuwa eneo la Pwani limeathirika sana tangu serikali ilipoanza kusafirisha mizigo kwa SGR kwani biashara nyingi zimefungwa na maelfu ya watu kufutwa kazi,” alisema Bw Ogolla.
Katika utafiti uliofanywa kati ya tarehe 27 Agosti na tarehe 14 Septemba mwaka huu, Bw Ken Ogolla, kiongozi wa kundi hilo la watafiti alisema biashara zinazohusiana na uchukuzi katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi kama vile vyumba vya kulala na stesheni za mafuta pia zimeathirika.
Ripoti hiyo imependekeza kutungwa kwa sheria inayoshinikiza serikali kukumbatia biashara huru ili wafanyibiashara waweze kuendelea na biashara zao ya kusafirisha mizigo.
Gavana Joho na viongozi waliohudhuria hafla hiyo walikashifu wakurungenzi wa Hamashauri ya Bandari (KPA) na ile ya ukusanyaji ushuru (KRA) kwa kutekeleza agizo hilo bila kufuata sheria.
“Agizo hilo lilitolewa na wakuu wa KPA na KRA na hakuna sheria yoyote inayowapa fursa kufanya hivyo ndipo tunataka agizo hilo kusitishwa mara moja,” alisema Gavana Joho.
Kitega uchumi
Bandari ya Mombasa imekuwa kitega uchumi kwa wakazi wa eneo la Pwani hasa wa Mombasa lakini amri mbali mbali zinazotekelezwa na Wizara ya Uchukuzi zimeathiri uchumi na maelfu ya wakazi kupoteza kazi zao.
Ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ulipokelewa kwa furaha na wakazi pamoja na viongozi wa Pwani lakini athari zake zimekuwa nyingi kwa biashara kuanzia kampuni za kusafirisha mizigo, maajenti wa kukagua mizigo hadi wamiliki wa mabasi yanayoelekea sehemu mbalimbali za nchi.
Zaidi ya kampuni 20 za CFSs ambazo zimewekeza takriban Sh12.5 bilioni katika mji wa Mombasa zimelazimika kufunga huku maajenti wakilazimika kuhama hadi eneo la Embakasi, Nairobi ambapo mizigo yote inasafirishwa kwa sasa kutoka bandarini Mombasa kutumia SGR.
Tangu mizigo yote kuanza kusafirishwa kwa reli ya SGR mwaka mmoja uliopita, wamiliki wa matrela 800 waliokuwa wakiendesha biashara ya kubeba mizigo wamelazimika kutafuta kazi mbadala kwani reli hiyo hubeba zaidi ya kontena 1200 kila siku na hivyo kukosesha kazi wamiliki wa malori.