Habari

SHA ni mpango bora zaidi kuwahi kuonekana nchini, serikali za awali hazikufua dafu – ODM

Na ERIC MATARA March 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimeunga Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF), ambayo imelaumiwa kwa kuvuruga huduma za afya nchini ikisema inaleta mageuzi ya kuafikia ufadhili wa Afya kwa Wote (UHC).

Hata hivyo, chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga kinaitaka serikali kurekebisha changamoto za kiteknolojia ambazo zimekumba utekelezaji wake.

Mwenyekiti wa ODM, Gladys Wanga, amepuuza miito ya kurejeshwa kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) akisema SHIF ni bora zaidi katika kutatua tatizo la ufadhili wa afya kwa wote nchini.

Bi Wanga alisema kwa sasa, mpango huo unakabiliwa na matatizo makubwa ambayo yanahitaji kushughulikiwa kwa haraka.

“SHIF ni mpango bora zaidi wa matibabu ambao tumewahi kuwa nao kama nchi. Serikali za awali zilishindwa kutimiza UHC, lakini hili ni jaribio la kijasiri la kuufanikisha,” Bi Wanga alisema kwenye NTV na Nation FM wakati wa kipindi cha asubuhi cha ‘Fixing The Nation’.

Alitoa wito kwa serikali kushughulikia changamoto za utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kukatika kwa mfumo mara kwa mara na ucheleweshaji wa malipo kwa vituo vya afya.

“Ikiwa tutarekebisha mapungufu, SHIF itakuwa mpango ambao tumekuwa tukihitaji kila wakati. Hatuhitaji kurejea NHIF kwani ulikuwa mfumo wa kibaguzi. Sikubaliani na mtu yeyote anayetetea kurejeshwa kwa NHIF,” aliongeza.

Licha ya hakikisho la serikali, SHIF imekosolewa vikali kutokana na hitilafu za mfumo, kucheleweshwa kwa malipo na kuongezeka kwa gharama za matibabu kwa Wakenya wanaotakiwa kulipia huduma licha ya kukatwa asilimia 2.75 ya mishahara kama ada ya bima hiyo.

Hii imesababisha wasiwasi kwamba mpango huo hautimizi malengo yaliyokusudiwa, huku viongozi wa upinzani, wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua na kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, wakiutaja kuwa kashfa.

Vituo vingi vya huduma za afya, hasa hospitali za kibinafsi, vimeacha kuhudumia wagonjwa chini ya SHIF kwa sababu ya kucheleweshwa kwa malipo kutoka kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).

“SHIF inakabiliwa na hatari ya kushindwa katika dhamira yake. SHIF haifanyi kazi inavyotarajiwa kutokana na changamoto hizi za kiufundi,” alisema kwa kusisitiza haja ya kuimarishwa kwa muundo kuhakikisha usawa katika michango.

“Watu wanaolipa zaidi michango wanapaswa kupata huduma bora zaidi. Tunahitaji mfumo unaolingana na kiasi ambacho mtu binafsi anachangia,” Bi Wanga aliongeza.

Wakenya kutoka sekta mbalimbali wameendelea kupaza sauti zao kuhusu SHIF. Wengi wanahisi kuwa mabadiliko kutoka NHIF hayakutekelezwa vizuri na kuwaacha mamilioni bila huduma bora za afya.