SHERIA ZA MICHUKI: Hakuna mjadala kuhusu sheria kwa matatu
BENSON MATHEKA na WINNIE ATIENO
WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Jumapili aliwapuuzilia mbali wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma wanaopanga kuondoa magari yao barabarani Jumatatu, akisisitiza kuwa msako wa magari mabovu ya uchukuzi wa umma utaendelea ilivyopangwa.
Magari mengi ya uchukuzi wa umma hayajatimiza mahitaji ya kisheria, na wananchi wametatizika Jumatatu kusafiri maeneo mbalimbali kote nchini msako ukianza.
Maafisa wa makundi ya wahudumu wa matatu walikuwa wamelalamikia hatua ya serikali ya kuwataka kutimiza sheria za trafiki za maarufu kama “Sheria za Michuki” kufikia Jumatatu na wakatoa wito kuwe na mashauriano zaidi kabla msako uanze.
Lakini akizungumza akiwa Kaunti ya Nakuru, Dkt Matiang’i alisema kuanzia Jumatatu, sheria za Mamlaka ya Taifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) na sheria za trafiki zitatekelezwa kitaifa na wakiukaji hawatahurumiwa.
“Katika suala hili hakuna majadiliano. Hatuwezi kuishi kama wanyama. Hatuwezi kukaa kitako na kutazama watu wakifa katika barabara zetu. Tunapaswa kuishi maisha yanayoheshimu sheria. Hii ndiyo sababu wizara itahakikisha sheria za uchukuzi zitatekelezwa katika barabara zetu kuanzia Jumatatu,” alisema Bw Matiang’i.
Kulingana naye, sheria hizo zilizoanza kutumika 2003 chini ya aliyekuwa waziri wa uchukuzi wakati huo marehemu John Michuki, zinalenga kudumisha usalama barabarani na kuzuia ajali ambazo zimesababisha maelfu ya Wakenya kuaga dunia na wengine kulemaa.
Sheria hizo zilitekelezwa kwa muda mfupi kisha kukawa na utepetevu uliowapa wahudumu wa magari ya umma uhuru uliosababisha barabara kuwa mitego ya vifo kwa wananchi.
Uamuzi wa wamiliki na wahudumu kusitisha huduma zao leo ni dalili kwamba Wakenya wamekuwa wakiabiri magari hatari kwa maisha yao.
Naibu Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Wamiliki wa Matatu, Bw Ali Bates, alikiri ni magari machache tu ambayo yametimiza kanuni za sheria za trafiki.
Kulingana naye, karibu asilimia 90 ya magari ya umma hayajatii sheria za trafiki na yataondolewa barabarani, akieleza kuwa kile kitakachofanyika leo si mgomo bali wanataka kuhakikisha magari yao yamo katika hali inayotakikana kisheria.
“Hatugomi bali magari yataondolewa barabarani kutokana na ukosefu wa mikanda ya usalama madukani. Ni magari machache ambayo yamefanikiwa kutekeleza mahitaji ya sheria za trafiki,” akasisitiza Bw Bates, akitoa mfano wa hali ilivyo Mombasa.
Bw Bates alisema wamiliki wa matatu wanasubiri mikanda hiyo ili waiweke na kuendelea na kazi. Magari pia yanahitajika kuwa na vidhibiti mwendo ambavyo haviwezi kuvurugwa na madereva wanaopenda kuendesha magari kwa kasi ya juu kuliko inavyoruhusiwa.
Dkt Matiang’i alisema wadau wote katika sekta ya uchukuzi wakiwemo madereva na abiria lazima wafuate sheria hizo kuanzia leo, ishara kuwa abiria hawatasazwa kwenye msako huo hasa kuhusu mahitaji ya kujifunga mkanda na kutopanda magari yaliyojaa.
“Ni lazima usalama katika barabara zetu udumishwe. Tumekuwa tukitoa ripoti za ajali ambazo zimeua Wakenya wasio na hatia na wengine kujeruhiwa. Lazima hizi ajali zikomeshwe,” alisema.
Kulingana na Dkt Matiang’i msimu huu wa sherehe za mwisho wa mwaka ambapo watu wengi husafiri, ni lazima sheria zifuatwe kulinda maisha yao.
“Novemba, Desemba and Januari ni miezi ambayo huwa na watu wengi wanaosafiri na hatutaki kupoteza maisha,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati ya bunge la kitaifa ya uchukuzi, Bw David Pkosing aliunga mkono hatua ya Dkt Matiang’i kuhakikisha usalama barabarani.