Habari

SHERIA ZA MICHUKI: Msako sasa waingia hongo

November 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

MWANGI MUIRURI, CECIL ODONGO Na WINNIE ATIENO

POLISI wanaoendesha msako dhidi ya matatu zinazokiuka sheria za trafiki maarufu kama “Sheria za Michuki” wameshutumiwa kwa madai ya kutumia shughuli hiyo kupokea hongo.

Wahudumu waliozungumza na Taifa Leo jijini Nairobi Jumanne, walieleza kuwa polisi hao wanawahangaisha na hatimaye kuwaitisha hongo ili waweze kuruhusiwa kuendelea kuhudumu.

“Wananasa magari na kuagiza yapelekwe vituo vya polisi hata bila ukaguzi wowote. Unapofika kituo cha polisi hauwezi kutoka kama hujalipa hongo,” walisema madereva jijini Nairobi.

Madereva hao walidokeza kuwa polisi wanaitisha hongo ya hadi Sh5,000 ili kuruhusu gari kuendelea kuhudumu.

“Ukweli ni kwamba sisi tumerejea barabarani baada ya kuhakikisha tumetimiza masharti yote ila sasa polisi wanatafuta makosa ambayo ni madogo sana kutuadhibu. Wenzangu wawili walikamatwa asubuhi na kuachiliwa baada ya kutoa hongo ya Sh5000,” akasema dereva wa magari ya Mwiki Sacco yanayohudumu kutoka kati mwa jiji la Nairobi hadi mitaa ya Kasarani na Mwiki.

Mwenzake kutoka Lucky Transporters naye alilalamikia ubovu wa mikanda ya usalama wanayonunua na gharama kubwa za kuhakikisha kila hitaji la sheria za barabarani linatimizwa kwa upande moja, na tamaa ya pesa ya polisi kula rushwa kwa upande mwingine.

“Hivi vitu tunaambiwa tuweke vinatugharimu pakubwa ilhali ni feki. Bei ya mshipi imepanda kutoka Sh200 hadi Sh800 na tayari nimelazika kununua mishipi mitano baada ya ile niliweka juzi kukatika,” akasema dereva huyo.

Afisa wa trafiki alitetea hatua ya magari kupelekwa kwenye vituo akisema ni vigumu kukagua magari hayo barabarani.

Ripota wetu pia alishuhudia polisi akipokea hongo kutoka kwa dereva wa matatu kwenye kituo cha ukaguzi Kaunti ya Murang’a.

“Matatu ilisimamishwa na sikuwa nimefunga mshipi kwa sababu ulikuwa na kasoro. Afisa wa polisi alikagua na kuona mikanda haikuwa sawa lakini hakushughulika. Kisha alienda upande wa dereva akapewa noti ya Sh200 na tukaendelea na safari,” alisema mwandishi wetu.

Duru zilidokezea Taifa Leo kuwa ulaji hongo unaendelea kama kawaida, lakini kile kimebadilika ni kuwa kiwango cha rushwa inayolipwa kimepanda kwa asilimia kubwa.

“Kile kimefanyika kwenye msako huu ni kuongezeka sana kwa kiwango cha hongo. Msako huu ukiisha polisi wengi hasa wakubwa watakuwa mamilionea,” alisema mdokezi katika idara ya usalama.

Alieleza kuwa kuna baadhi ya mashirika ya magari (Sacco) ambayo yametoa mamilioni kama hongo kwa maafisa husika katika idara ya trafiki, NTSA na Wizara ya Uchukuzi ili kulindwa.

“Wenye matatu wanaoumia ni wale Sacco zao hazijagundua mbinu mpya ya ufisadi. Wale wamelipa hongo wanapigiwa simu na kujuzwa mahala kuna misako ili waepuke kunaswa, wapunguze kasi ama wasibebe abiria zaidi. Wanaolipa wanalindwa na wakubwa hata kama hawajatimiza kanuni za NTSA,” alisema afisa huyo.

Msemaji wa polisi, Charles Owino hakujibu simu wala SMS tulizomtumia kuhusu madai hayo ya hongo.

Wenye magari yakiwemo ya abiria pia wamelalamika kuwa polisi wanatumia msako huo kuhangaisha wananchi. Katika eneo la Thika, waendeshaji magari yaliyonaswa Jumatatu walilalamika kunyimwa dhamana ama kupigwa faini za papo hapo kama ilivyokuwa imetangazwa awali.

Hata hivyo hali ya kawaida ya usafiri ilianza kurejea jijini ingawa magari bado yalikuwa machache, utingo na madereva wakisema kwamba baadhi wanaogopa kurudi barabarani ili yasinaswe kwa kile walisema ni makosa ya kutafutia.

Mjini Mombasa hali ilisalia jinsi ilivyokuwa Jumatatu baada ya wamiliki magari kushikilia kwamba kamwe hawatarejesha magari yao barabarani.

Wahudumu walisema Serikali haitoi mwelekeo wazi kuhusu kanuni wanazopasa kutimiza.

“Tunataka dereva na kondakta waadhibiwe kivyao wakipatikana na makosa wala yasilimbikiziwe kwa mwenye matatu na sacco. Kila mmoja abebe msalaba wake,” akasema Mshirikishi wa wamiliki wa matatu tawi la Pwani Bw Salim Mbarak.