Habari

Shika adabu yako, Kuria amwambia Sudi

July 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria amepuuzilia mbali madai ya mwenzake wa Kapsaret, Oscar Sudi aliyemtaka Rais Uhuru Kenyatta kujiuzulu kwa kile alikitaja ni kushindwa kudumisha uongozi bora nchini.

Mnamo Jumatano, Bw Sudi alidai pengine anaweza kuliongoza taifa hili kwa njia nzuri kuliko Rais Kenyatta endapo anaweza kupata fursa hiyo na akampendekeza Bw Kuria kuwa naibu wake.

Sasa kwenye ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa mtando wa Facebook, Bw Kuria amemjibu Bw Sudi akimwonya dhidi ya kumwingiza katika “ujinga wako.”

“Nakuonya Oscar Kipchumba Sudi ukome kuniingiza katika ujinga wako. Mimi huendesha vita vyangu mahakamani kwa unyamavu na kwa kuheshimu sheria na Katiba. Hakuna anayenisaidia na sitaki nisaidiwe,” akaandika Bw Kuria.

Akaongeza: “Masuala ambayo ulirejelea yako mahakamani na hivyo kauli zako ni kinyume cha sheria kwa sababu yanaingilia kesi iliyo kortini. Hata hivyo, nakuhurimia kwa sababu matamshi yako yanafanya watu wengi kushangaa kile utakachofanya endapo utaruhusiwa kukaribia umbali wa kilomita 50 kutoka Ikulu miaka mingi ijayo.”

Bw Sudi alitoa matamshi hayo kwenye kikao na wanahabari nyumbani kwake katika Kaunti ya Uasin Gishu alipokosoa kukamatwa na kushtakiwa kwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na Katibu wa wizara hiyo Kamau Thugge.

“Mbona Rotich anashikwa kwa tuhuma za ufisadi ilhali amehudumu kama waziri kwa zaidi ya miaka saba? Mbona wakati huu ndio inabainika kuwa yeye ni fisadi. Rotich amesingiziwa makosa kwa lengo la kufanikisha ajenda fulani ya kisiasa. Hatutakubali mtumishi wa serikali mwadilifu kama huyo kutolewa kafara kwa vita vya wengine,” akasema Sudi.