Habari

Shirika lazindua jukwaa kukabili unyanyasaji wa kijinsia mitandaoni

Na LUCY KILALO November 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHIRIKA la KICTANet kwa ushirikiano na Meedan limezindua jukwaa la kidijitali litakalowawezesha watu kupiga ripoti kuhusu dhuluma na unyanyasaji katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Jukwaa hilo linalofahamika kama Check Tip Line: MLINZI linalenga kukusanya taarifa kuhusiana na unyanyasaji wa kijinsia unaoendeshwa mitandaoni (TFGBV) hasa kwa kutumia lugha ya Kiswahili na Sheng.

Juhudi hizo zimefuatia utafiti uliofanywa awali na KICTANet kuhusiana na maneno ya Kiswahili na Sheng ambayo yamekuwa yakitumika mitandaoni kuendeleza unyanyasaji kwa kutumia majukwaa hayo ya kiteknolojia.

“Kenya inajivunia kuwa mbele katika mageuzi ya dijitali Afrika. Ikiwa na watumiaji 15 milioni wa mitandao na jamii inayokuwa kwa kasi ya mitandaoni, nchi yetu inaonyesha hatua kubwa katika masuala ya dijitali na uvumbuzi. Hata hivyo, hatua hizi zinamaanisha uwajibikaji zaidi. Nyenzo zinazotumika kutuunganisha na kutuwezesha, ndizo mara nyingi, hutumika kudhuru na kunyamazisha, hasa wanawake na wengine waliokandamizwa,” alisema kinara wa Mpango wa Haki za Kidijitali za Wanawake katika Shirika la KICTANet, Bi Cherie Oyier alipozindua rasmi jukwaa hilo, Ijumaa Novemba 7, 2025.

“Utafiti wetu kuhusiana na dhuluma za kijinsia mtandaoni (kuanika uhangaishaji wa watu) ulituonyesha kuwa asilimia 63 ya wanawake wa maeneo ya mijini na 37 wa mashambani, wamepitia aina ya unyanyasaji au dhuluma mitandaoni. Nambari hizi si takwimu tu, zinawakilisha maisha halisi, maumivu halisi na changamoto ambazo lazima tuzikabili moja kwa moja.”

Shirika la KICTANet linaeleza kuwa dhuluma hizo za mitandaoni (TFGBV) hujitokeza kwa njia nyingi, ambazo ni watu kukuandama mitandaoni, kutuma picha zako za faragha bila idhini na hata kuiba utambulisho wako mitandaoni.

Juhudi hizo, anasema Bi Oyier, zinalenga pia kuhamasisha jamii kuchangia katika uhakikishaji wa majukwaa salama ya kidijitali, mbali na kukusanya data ambazo zitasaidia kushinikiza uundaji wa sera za kutoa usaidizi kwa waathiriwa wa dhuluma hizo.

Aliongeza kuwa waathiriwa pia wanahitaji msaada wa kisaikolojia kwa kuwa dhuluma hizo za mitandaoni huishia kuwatatiza pakubwa kiakili.

Katika juhudi zake, KICTANET pia ilieleza kuwa inalenga kushirikiana na mitandao hiyo ya kijamii kuwa na utaratibu ambapo waangalizi wake wa maudhui yanayowasilishwa kwa Kiswahili, watakuwa na uwezo wa kuyatambua yale yanayoendeleza unyanyasaji na kuyazima ili yasiendelee kusambazwa.