Shule hazipumui, zimelowa madeni wakuu wakipanga kufunga muhula mapema
OFISI ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeweka wazi changamoto zinazokumba shule nyingi za umma nchini, huku nyingi zikikumbwa na mzigo mkubwa wa madeni kutokana na ufadhili mdogo kutoka kwa Serikali.
Katika ripoti maalumu iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC), Mkaguzi Mkuu Nancy Gathungu alifichua kuwa, Serikali ya Kitaifa haijakuwa ikitengea shule za umma fedha za kutosha.
Haya yanajiri huku madai ya wanafunzi na shule hewa zinazotumiwa pesa yakiibuka na walimu wakuu wakiwazia kufunga shule mapema muhula huu kwa kukosa pesa baada ya serikali kuchelewesha mgao wa muhula wa pili.
Kulingana na ukaguzi uliofanyika kati ya mwaka wa kifedha wa 2021 hadi 2024, shule za umma zilikosa kupata ufadhili wa jumla ya Sh117 bilioni, huku shule za upili zikiathirika zaidi.
Akizungumza mbele ya kamati inayoongozwa na Mbunge wa Butere, Tindi Mwale, Mkurugenzi wa Ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu, Justus Okumu, alisema mgao wa shule za upili ulipungua kwa Sh71 bilioni katika kipindi hicho cha miaka minne.
Mgao wa Sekondari Msingi ulipungua kwa Sh39.9 bilioni huku shule za msingi zikikosa Sh14 bilioni.
“Tatizo kuu linalokumba shule za umma ni ukosefu wa ufadhili wa kutosha. Wizara huandaa bajeti kwa shughuli mbalimbali za shule, lakini mara kwa mara hupunguzwa. Hali hii husababisha baadhi ya shughuli kusitishwa au kutekelezwa nusu nusu, hivyo kuchangia kuongezeka kwa madeni,” Okumu alieleza kamati.
Katika ukaguzi huo, Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Usimamizi wa Elimu (NEMIS) ulilaaniwa kwa kuonyesha idadi ya wanafunzi isiyolingana na idadi halisi shuleni.
Mfumo huo ulilaumiwa kwa kusababisha baadhi ya shule kufadhiliwa chini ya kiwango, huku nyingine zikipokea fedha kupita kiasi.
Iliibuka kuwa, shule 33 zilitumiwa pesa huku zile halisi zikihangaika kuendesha shughuli zake.
Taarifa hizi za kushangaza ziliwasilishwa na Dkt Gathungu katika ukaguzi maalumu kuhusu mgao na miundombinu shuleni, ambao uliwasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC).
Wizi huo mkubwa uligunduliwa katika miaka ya kifedha kuanzia 2020 hadi 2024, huku ikibainika kuwa shule za umma zilikuwa zimepunguziwa ufadhili.
Aidha, ukaguzi huo ulipinga mfumo wa sasa wa kutoa mgao kwa shule, ukisema kuwa si wa haki na unaleta tofauti kubwa ambazo huwafaidi wanafunzi kutoka familia zenye uwezo badala ya wanaohitaji zaidi.
Bw Okumu alisema baadhi ya shule zilizopokea fedha haziko kabisa, wala hakuna majengo wala miundombinu mashinani isipokuwa akaunti za benki pekee.
“Shule hewa ni zile zinazoonekana katika mfumo wa serikali, lakini tulipofika mashinani hatukuzikuta. Zinapokea fedha lakini maafisa wa elimu hawakuweza kutuonyesha zilipo,” alisema.
Ukaguzi huo maalum ulieleza kuwa kiwango cha fedha kinachotengwa kwa kila mwanafunzi kwa sasa hakizingatii mahitaji tofauti ya shule na mazingira yao, hivyo basi kuufanya mfumo huo kuwa usio wa haki.
Ingawa orodha ya shule zilizopokea mgao haikuwekwa wazi katika kikao hicho, kamati hiyo iliagiza Ofisi ya Mkaguzi Mkuu kuwasilisha taarifa kamili.
Ripoti hiyo ya ukaguzi ilionyesha kuwa shule tatu za upili zilikuwa zikitumia akaunti moja ya benki na kupokea jumla ya Sh103.3 milioni kama mgao, jambo lililoibua wasiwasi kuhusu utumiaji na usimamizi wa fedha hizo.