Shule nyingi za msingi Gatundu Kaskazini zahitaji ukarabati maalum
Na LAWRENCE ONGARO
KUNA haja ya kuboresha shule za msingi katika eneo la Gatundu Kaskazini ili wanafunzi wapate matokeo ya kuridhisha, amesema kiongozi.
Mbunge wa eneo hilo Bi Anne Wanjiku Kibe alisema Jumatatu kwamba amezindua miradi ya kukarabati shule zote 60 katika eneo lake la uwakilishi baada ya kupata shule nyingi zikiwa katika hali mbovu kimazingira.
“Shule zikiwa katika hali hiyo hata masomo huwa ni ya kutilia shaka. Hata walimu mara nyingi huwa hawana motisha ya kufunza kwa kwa bidii,” alisema Bi Kibe.
Alisema kwa muda wa miaka mitatu ijayo anapanga kuona ya kwamba amekarabati shule 30 kwa mtindo wa kisasa ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kujibiidisha zaidi wawapo madarasani.
Alizuru shule tatu za msingi na moja ya upili kwa lengo la kukarabati madarasa yake ili kubadilisha sura ya shule hizo.
Shule ya kwanza kuzuru ya msingi ilikuwa Mutuma ambapo imefanyiwa marekebisho makubwa .
“Ninafahamu vyema kuwa shule hii ilifanya vibaya kwenye mtihani wa darasa la nane wa 2018, lakini sura mpya ya shule hii sasa itabadilisha msimamo wa matokeo yajayo,” alisema Bi Kibe.
Vifaa
Alitaja baadhi ya vifaa muhimu na akasema kukosekana kwake huathiri vibaya matokeo shuleni.
Alitaja ukosefu wa madawati, vyoo vya kisasa, umeme, maji, na vitabu vya kusoma kwa wanafunzi.
“Wakati huu nitafanya juhudi kuona ya kwamba nimetumia vyema fedha za CDF ili kunufaisha wanafunzi walio katika shule za msingi. Hatua hiyo nitachukua mara moja bila kupoteza muda,” alisema Bi Kibe.
Wakati huo pia alizuru shule ya msingi ya Muirigo ambapo aliwahakikishia walimu misaada yote wanayohitaji kama shule.
“Ninajua mnapitia changamoto tele; nami kama mbunge wenu nitafanya juu chini kuona wanafunzi na walimu wanaongezwa motisha ili wazidi kujiendeleza zaidi,” alisema Bi Kibe.
Katika shule ya upili ya Kanjuku Mixed Day Secondary alisema kuna changamoto ya kuwa na walimu wachache na kwa hivyo atawasiliana na afisi husika katika Wizara ya Elimu jijini Nairobi ili waongeze walimu zaidi.
Alisema ni vyema wanafunzi kupata walimu wa kutosha ili kuboresha maswala ya elimu katika eneo hilo.
Aliwahimiza pia wakazi kushirikiana naye ili aweze kufanikisha mipango yake ya miaka mitatu ijayo.