Shule zafunguliwa walimu wakihofia kufukuzana tena na serikali kuhusu pesa
SHULE zinafunguliwa wiki hii kwa muhula wa pili, huku walimu wakuu wakitoa wito kwa serikali kutoa fedha bila kuchelewa ili kuepuka misukosuko inayoshuhudiwa mara kwa mara wakati wa muhula huu mrefu zaidi wa kalenda ya masomo.
Katika muhula huu, serikali pia inatarajiwa kutangaza uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na shule za Sekondari Pevu mwaka ujao.
Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA), Bw Willy Kuria, ameitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha pesa zinazotengewa wanafunzi ni 22,000 na zitumwe kwa shule mapema ili kusaidia kupanga shughuli za ziada ambazo hutawala muhula huu.
“Hali ilikuwa mbaya sana, tulikaribia kufunga shule kabla ya wakati kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Tunapofungua shule, Sh2,300 za muhula wa kwanza hazikutolewa ili kuwa Sh11,000. Tafadhali toeni pesa hizo kabla ya kutuma pesa za muhula wa pili,” alisihi Bw Kuria.
Mkuu huyo wa shule ya upili ya Murang’a alisema ukosefu wa fedha umesababisha shule nyingi kukosa kushiriki katika shughuli za ziada, jambo ambalo hufanya wanafunzi kusababisha ghasia.
“Muhula huu huwa na shughuli nyingi za ziada. Wakikosa kushiriki, hiyo huwa dalili ya matatizo. Mara nyingi tunakosa kushiriki katika shughuli hizo kwa sababu ya ukosefu wa fedha,” alieleza.
Bw Kuria alisema muhula wa pili ni mrefu na muhimu zaidi kwa sababu walimu hujitahidi kukamilisha silabasi.
“Ni muhula wenye shughuli nyingi unaoamua ikiwa watahiniwa watafaulu au kufeli mitihani yao ya kitaifa,” alibainisha.
Aliongeza: “Ni muhula ambapo ghasia kama migomo hutokea kwa sababu ya mitihani ya majaribio. Wanafunzi wengine huwa hawajajiandaa na hivyo kuzua fujo. Wakuu wa shule wanapaswa kuwa macho.”
Muhula huo unaanza Aprili 28 na utaendelea kwa wiki 14 hadi Agosti 1.
Kwa mujibu wa ratiba ya mwaka wa masomo 2025, wanafunzi watapata mapumziko ya katikati ya muhula kwa siku tano kuanzia Juni 25 hadi Juni 29.
Shule zitafungwa tena mwezi Agosti kwa wiki tatu, kuanzia Agosti 4 hadi Agosti 22, kabla ya muhula wa tatu kuanza.Katika mahojiano na Taifa Leo, Waziri wa Elimu Bw Julius Ogamba alihakikishia kuwa atahakikisha fedha zinatumwa shuleni kwa wakati.