Shule zafungwa wiki hii baadhi zikikosa kabisa mgao wowote
SHULE zinapofungwa wiki hii kwa likizo ya muda wa miezi miwili, Wizara ya Elimu bado inakabiliwa na changamoto kufuatia mgao wa elimu kutotolewa kwa wakati kwa shule mbalimbali.
Haya yanatokea huku Hazina Kuu ya Fedha na Wizara ya Elimu zikishirikiana kubadilisha kalenda ya ufadhili kutoka Januari – Disemba hadi Juni ili ioane na mwaka wa fedha wa serikali.
Hadi sasa serikali imetoa Sh22.1 bilioni kama mgao wa kufadhili elimu kwa shule za msingi na zile za upili.
Baadhi ya shule zilikosa ufadhili wakati ambapo mchakato wa kuhakiki na kuondoa shule feki zenye wanafunzi hewa ulikuwa ukiendelea.
Kwa mujibu wa Katibu katika Wizara ya Elimu Julius Bitok, shule 18,000 kati ya zile 23,000 zimepokea mgao wao. Bado shule 5,000 zinahakikiwa.
Kuna shule 97,800 za umma ambapo 47,666 ni za chekechea, 35,570 za msingi kisha 10,752 za sekondari.
“Shule kadhaa hazijapata mgao kutokana na tofauti kwenye data walizowasilisha kuhakikiwa. Bado data zao zinaangaliwa kabla ya fedha kutolewa,” akasema Profesa Bitok.
Profesa Bitok alifichua kuwa Wizara ya Elimu imetoa Sh10.4 bilioni kwa Wizara ya Elimu katika shule za sekondari ambapo Sh10.1 bilioni zimetumwa kwa shule.
Kwa shule za sekondari za chini, hazina kuu imetoa Sh4.8 bilioni kati ya Sh5.6 bilioni huku Sh800 milioni ambazo zimesalia zikitarajiwa kutumwa kwa shule.
“Ripoti itaandaliwa ambayo itaonyesha tofauti kwenye data iliyowasilishwa. Wakurugenzi wa elimu kwenye kaunti na kaunti ndogo wanafanya kazi na shule ili kushughulikia utata ambao umetokea,” akasema Profesa Bitok.
“Imebainika kuwa baadhi ya shule zina wanafunzi chini ya idadi ya wastani ya wanafunzi 45 ambao wanahitajika katika kila darasa kwa mujibu wa Wizara ya Elimu,” akasema Profesa Bitok.