Si lazima niwe Rais 2022 – Raila
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amekanusha madai kuwa anatumia mchakato wa kuleta maridhiano nchini (BBI) kumsadia kuingia Ikulu 2022 akisema, ni mpango wa kutengeneza mustakabali wa taifa hili kwa manufaa ya Wakenya wote.
Akiongea Jumamosi katika mkutano wa pili wa uhamasisho kuhusu yaliyomo kwenye ripoti ya BBI katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega, Bw Odinga alisema sio lazima awe Rais wa Kenya lakini akasisitiza kuwa sharti taifa hili liwe na rais bora 2022.
“Nilianzisha mpango huu wa BBI na Uhuru kwa manufaa ya taifa hili. Sio kwa manufaa ya Raila Odinga. Sio lazima Raila kuwa Rais wa Kenya, lakini sharti Kenya iwe na Rais bora,” akasema.
Huku akitoa historia ya handisheki kati yake na Rais Kenyatta, Bw Odinga alielezea matumaini kuwa BBI ni mchakato ambao utasaidia kuleta mageuzi ya uongozi nchini ambayo hayawezi kufanikishwa kupitia katiba ya sasa.
Naibu Rais William Ruto na wanasiasa wanaounga mkono ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022 wamemsuta Bw Odinga kwa kuteka mchakato wa BBI kwa manufaa yake ya kisiasa.
Kulingana nao, kiongozi huyo wa upinzani anatumia msururu wa mikutano ya uhamasisho kuhusu yaliyomo kwenye ripoti ya BBI kama jukwaa la kuipigia debe azma yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tunajua ajenda yao. Mkutano wa Kakamega sio wa BBI bali ni wa ODM wenye lengo la kumfaidi Raila Odinga kisiasa. Hauna ajenda yoyote yenye manufaa kwa jamii ya Waluhya na Wakenya kwa ujumla,” akasema, kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Benjamin Washiali akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge juzi.
Lakini Jumamosi, Bw Odinga alitumia jukwaa la uwanja wa Bukhungu kufafanua kuhusu nguzo kadha za BBI kando na kuboresha uongozi wa nchi. Nguzo hizo ni pamoja na vita dhidi ya ufisadi, mageuzi katika mfumo wa uchaguzi, umoja wa kitaifa na uwepo wa usawa katika teuzi serikalini.
“Hii handisheki kati yangu na Uhuru inalenga kuleta manufaa mengi kwa Wakenya na imechangamsha mataifa mengi Afrika na ulimwengu kwa ujumla kwa sababu ya manufaa yake. Hii ndiyo maana juzi nilialikwa nchini Togo nifanikishe handisheki kati ya Rais na upinzani huko,” akasema.
Bw Odinga aliongeza kuwa ni kutokana na handisheki hiyo ambapo wamealikwa na Rais Kenyatta nchini Amerika mnamo Februari 4 na 5 mwaka huu kuhudhuria Hafla ya Maombi.
Naye Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alisema mkutano huo ulikuwa mradi wa Serikali wala sio wa chama cha ODM jinsi wapinzani wake wamekuwa wakidai.
“Nilipata amri kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kwamba, niandae mkutano huu. Kwa hivyo mkutano huu wa BBI ni mradi wa Serikali Kuu wala sio wa chama chochote, “akasema.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na magavana; James Ongwae (Kisii), John Nyagarama (Nyamira), Patrick Wangamati (Bungoma), Patrick Khaemba (Trans Nzoia), Cornell Rasanga (Siaya), Peter Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Cyprian Awiti (Homa Bay), Okoth Obado (Migori) na Dkt Wilbur Ottichilo. (Vihiga), Wycliffe Wangamati (Bungoma). Wengine walikuwa gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na mwenzake wa Kitui Charity Ngilu.
Pia alikuwepo Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, maseneta na wabunge kutoka eneo la magharibi na maeneo mengine ya nchi.
Kiogozi wa Amani National Congress Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya ambao awali walitangaza kususia mkutano huo pia walikuwepo.