Habari

Siasa za tabaka hili dhidi ya lile si nzuri, ODM yaambia Ruto

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE sita wa ODM Jumatatu walilaani ghasia zilizoshuhudiwa katika mji wa Kenol, Kaunti ya Murang’a ambapo watu wawili walifariki wakati wa ziara ya Naibu Rais William Ruto.

Hii ni baada ya kutokea mapigano kati ya kundi la vijana la wafuasi wa Dkt Ruto na wanachama wa kundi pinzani ambao walitaka kuvuruga mkutano huo.

Wakiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, wabunge hao wakiongozwa na kiongozi wa wachache John Mbadi walidai kuwa Dkt Ruto na wabunge wandani wake ndio walichochea ghasia hizo.

“Ruto ana hasira nyingi zaidi na uchu mkubwa wa kuwa Rais wa Kenya. Hii ndiyo maana anatumia mbinu yoyote kufikia lengo hilo. Kwa hivyo, anahitaji kudhibitiwa tukielekea katika uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema Bw Mohammed akisoma taarifa kwa niaba ya wenzake.

Bw Mbadi alisema Dkt Ruto anaendeleza kampeni hatari ya kuleta mgawanyiko kati ya wale anaowataja kama masikini na wale ambao anawataja kama matajiri, kampeni ambayo alisema inalenga kuchochea uhasama nchini Kenya.

“Hizi kampeni za mahasla na matajiri ni hatari kwa uthabiti wa taifa hili. Ruto anafaa kukomeshwa,” akasema mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM.

Bw Mbadi pia alidai kuwa Naibu Rais anapanga kuzuru Kisumu na maeneo mengine ya Nyanza kama vile Siaya, lakini akamuonya “kutosababisha fujo huko.”

“Ruto amekaribishwa Luo Nyanza lakini asilete vita huko kwani eneo hilo limeathirika kutokana na fujo za kisiasa kwa miaka mingi. Tunataka amani na utulivu chini ya mwavuli wa BBI,” akasema Mbunge huyo wa Suba Kusini.

Wengine walioandamana naye ni: Gladys Wanga (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Homa Bay), Antony Oluoch (Mathare), Jared Okello (Nyando) na Seneta Maalum Getrude Musuruve.