Sifuna kuzindua makao makuu ya chama na kampeni ya urais
SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anatarajiwa leo Ijumaa kuzindua makao makuu ya vuguvugu la Linda Mwananchi na kituo cha kuratibu kampeni zake za urais wa 2027.
Ofisi hizo ziko Lavington, Nairobi, na ni sehemu ya juhudi za kuimarisha vuguvugu hilo baada ya kupata chama cha The Equitable Party (TEP), ambacho kinabadilishwa jina kuwa Linda Mwananchi Movement.
Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema uzinduzi huo pia utahusisha kutangazwa kwa baadhi ya maafisa wa kitaifa wa chama hicho. Alisema orodha kamili itakamilishwa baadaye ili kutoa nafasi kwa wanachama wengine kujiunga.
Vuguvugu hilo lilimteua Bw Sifuna kuwa kiongozi wake na mgombea wake wa urais mnamo Septemba.
Miongoni mwa wanasiasa wanaotarajiwa kupewa majukumu muhimu ni Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo.
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na Gavana wa Siaya James Orengo, ambao walikuwa sehemu ya vuguvugu hilo, wameanzisha vyama vyao tofauti.
Bw Owino amepata Muungano Party na kukibadilisha jina kuwa The Mwananchi Party, huku Bw Orengo akizindua Liberal Democratic Party (LDP).
Bw Oundo alisema chama hicho kitapanga kongamano la kitaifa la wajumbe (NDC) Novemba 13 ili kukamilisha mabadiliko ya jina na kuthibitisha uongozi mpya.
Pia, kinapanga kufungua ofisi katika kaunti zote 47 kufikia Desemba na kuanzisha mfumo wa mtandaoni utakaowawezesha wanaotaka kuwania viti mbalimbali kuwasilisha maombi yao.
Baada ya uzinduzi wa Nairobi, vuguvugu hilo linapanga mkutano mkubwa wa kisiasa Kaunti ya Kwale Jumamosi.
Hatua hizo zinafuatia kutofautiana kwa Bw Sifuna na chama cha ODM, ambacho alikuwa katibu mkuu wake.
Utafiti wa TIFA uliochapishwa Julai ulionyesha kuwa asilimia 15 ya waliohojiwa walimuunga mkono Bw Sifuna iwapo angewania urais. Rais William Ruto alipata asilimia 24 katika utafiti huo.
Wakati wa uzinduzi wa TEP, Bw Sifuna alisema vuguvugu hilo linalenga kuangazia matatizo ya wananchi wa kawaida, ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, changamoto za wakulima, ushuru kwa wafanyabiashara wadogo na gharama ya elimu na matibabu.
Alisema chama hicho kinataka vijana na wanawake washirikishwe zaidi katika maamuzi ya kisiasa na kuweka mbele uwajibikaji, huduma kwa wananchi na kuheshimu Katiba.
Vuguvugu hilo pia linatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wengine wa upinzani kuhusu uwezekano wa kushirikiana kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027.