Siku ya utalii duniani yaadhimishwa matumaini ya sekta kuimarika yakiongezeka
Na MISHI GONGO
MAELFU ya watu wamefurika katika bustani ya Mama Ngina kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani.
Sherehe hizo zilizoandaliwa na serikali ya Kaunti ya Mombasa zilihusisha waimbaji kutoka nchini wakitumbuiza
Miongoni mwa wasanii waliotarajiwa kunogesha shamrashamra hizo ni Tanasha Donna, Otile Brown, Masauti miongoni mwa wasanii wengine.
Sherehe hizo zimeanza kwa uendeshaji basikeli ambapo watu zaidi ya 400 wameshiriki wakiwa wametoka maeneo mbalimbali kote nchini.
Kisha baadaye waendeshaji baiskeli hao wamezuru maeneo mbalimbali ya kijamii katika mji huo yakiwemo Kengeleni, Ngome ya Fort Jesus, Pembe za Ndovu na hatimaye kukusanyika katika bustani ya Mama Ngina Waterfront.
Kulingana na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho ni kwamba wameanzisha utalii wa michezo ili kuimarisha afya za wakazi wa Mombasa, kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na magari na kupunguza msongamano wa magari ambao unashuhudiwa kila siku.
“Tunataka kuanzisha utalii wa michezo katika mji wetu ili kuboresha afya za wakazi na wageni wanaofika hapa, lakini pia kuongeza kipato,” amesema.
Sherehe hiyo imehudhuriwa na gavana Joho, seneta Mohammed Faki, mbunge wa Likoni Mishi Mboko, Badi Twali (Jomvu), Omar Mwinyi (Changamwe ), wawakilishi wadi, mafisa wa afya na utalii katika kaunti hiyo pamoja na washika dau mbalimbali katika sekta ya utalii.
Wengi waliopata fursa ya kuhutubu wamesema michezo itasaidia kufufua utalii katika eneo hilo.
Utalii ulidorora kutokana na kuzuka kwa janga la corona.