Habari

Soko la Gikomba ni ardhi ya umma, Ruto sasa aonya watu wanaolimezea mate

Na KEVIN CHERUIYOT January 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MVUTANO wa muda mrefu kuhusu umiliki wa ardhi ya thamani kubwa katikati ya Kaunti ya Nairobi, inayotumiwa kama soko kubwa zaidi la wazi Afrika Mashariki – Soko la Gikomba, unatarajiwa kufikia tamati baada ya serikali ya kitaifa kuingilia kati.

Katika kikao kilichofanyika Ikulu wiki hii na kuhudhuriwa na viongozi wa masoko pamoja na madiwani katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Rais William Ruto alitangaza kuwa soko hilo ni mali ya serikali.

Tamko hilo linatarajiwa kuleta afueni kwa mamia ya wafanyabiashara ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakipata hasara kutokana na matukio ya visa vya moto unaoteketeza vibanda vyao.

“Nawahakikishia kuwa Gikomba ni ardhi ya umma, na hatuwezi kusema hivyo bila kuwa na stakabadhi kamili. Lazima kuwe na stakabadhi zinazoonyesha wazi kuwa Gikomba ni mali ya umma,” alisema Rais.

Aliagiza Katibu katika Wizara ya Ardhi Nixon Korir kushirikiana na Waziri wa Ardhi Alice Wahome ili kuharakisha mchakato wa kupata stakabadhi na hatimaye kutoa hatimiliki.

Ukosefu wa hati miliki umetajwa kuwa chanzo kikuu cha mikasa ya mara kwa mara ya moto katika soko hilo kwa miaka mingi.

Katika visa vya hivi majuzi, wafanyabiashara wamewalaumu watu wanaodai kumiliki ardhi hiyo kwa kupanga visa vya moto.

Mbali na suala la hatimiliki, serikali ya kitaifa imeanza kujenga soko la kisasa la kudumu Gikomba na kulizungushia ukuta wa usalama. Pia, kituo cha zimamoto kimejengwa karibu na soko hilo.