Habari

Sonko atabasamu mahakama ya Afrika Mashariki ikikubali kesi yake

Na  Sam Kiplagat December 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), imekubali kusikiliza kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kuhusu uamuzi wa korti ya Kenya wa kumzuia kushikilia wadhifa wa umma.

Hatua hiyo ni ushindi wa kiasi kwa Bw Sonko ambaye anajaribu kuondoa vizingiti vya kisiasa alivyowekewa na mahakama ya Kenya.

EACJ ilisema ina mamlaka ya kusikiliza na kuamua vipengele vya kesi ambavyo vinahusu ukiukaji wa mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao Kenya imeidhinisha.

“Mlalamishi amethibitisha kuwa Mahakama ya Juu, huenda ilikosa kuzingatia kanuni za utaratibu, ambazo ikithibitishwa, itakuwa ni ukiukaji wa Kifungu cha 25 cha katiba ya Kenya na Kifungu cha 6 na 7 cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” mahakama hiyo inayoongozwa na Jaji Yahane B.

Masara ilisema Kulingana na EACJ, Sonko ambaye alitimuliwa mwaka wa 2020, alionyesha kwamba atapata madhara yasiyoweza kurekebishwa ikiwa maagizo anayotaka hayangetolewa.

Hii ni kwa sababu uamuzi wa Mahakama ya Juu ulimzuia kushiriki katika siasa hatua ambayo ina madhara makubwa.

“Athari katika haki zake za kisiasa, sifa na uwezo wa kujihusisha na huduma za umma inaonyesha madhara yasiyoweza kurekebishwa yanayoweza kumpata,” ilisema mahakama hiyo.

Sonko aliondolewa kama gavana wa Kaunti ya Nairobi mnamo Novemba 26, 2020 na akawasilisha kesi kadhaa katika Mahakama Kuu kupinga kutimuliwa kwake.

Kesi zake zilitupiliwa mbali na hatimaye kesi ikaishia katika Mahakama ya Juu.Aliwasilisha kesi hiyo mbele ya EACJ akidai kuwa katika uamuzi wa mwisho, Mahakama ya Juu ilimzuia kikamilifu kushiriki uchaguzi au kushikilia wadhifa wa umma.

Alidai kesi katika Mahakama ya Juu iliendeshwa kwa namna ambayo ilikiuka utawala wa sheria, haki asilia na kanuni, uwazi na uwajibikaji.

Alisema kuwa Jaji Mkuu Martha Koome alitoa maoni hadharani kuhusu kesi yake kabla ya uamuzi huo kutolewa, na hivyo kuhujumu hitaji la kutopendelea.

Vitendo hivyo alisema vinakiuka ibara ya 6(d) na 7(2) ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA