Sonko atikisa ngome ya Kalonzo na chama kipya
KUZINDULIWA kwa chama kipya cha kisiasa cha aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko, National Economic Development Party (NEDP), kumesababisha taharuki ya kisiasa Ukambani huku Wiper Patriotic Front (WPF), kilicho maarufu eneo hilo, kikijaribu kupunguza hofu kwamba kurudi katika siasa kwa Sonko kunaweza kuathiri hesabu za Kalonzo Musyoka katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Bw Musyoka ambaye ni Kiongozi wa WPF, anakabiliwa na mabadiliko mapya ya kisiasa katika ngome yake, jambo lililosababisha chama hicho kuweka mkakati wa kujilinda, huku baadhi ya washirika wake wakihofia nia, na athari zinazoweza kutokea kutokana na kurudi kwa Sonko katika siasa.
Licha ya kukabiliwa na mashtaka ya kisheria na changamoto za kisiasa, Sonko bado ana nguvu kisiasa zinazoweza kuvuruga uthabiti wa kisiasa.
Hii ndiyo sababu, licha ya Wiper kuepuka kuonyesha hofu hadharani, kinafikiria kimya kimya jinsi ya kumkabili.
“Chama hiki cha Sonko ni tishio kubwa kwa chama chetu hasa Ukambani na hapa Nairobi. Uongozi wa juu wa Wiper unahitaji kuwa makini. Ima tushughulikie chama hiki kipya kwa nguvu zote au tuketi pamoja na Sonko. Tubadilishe mkakati ili Wiper ibaki maarufu hasa katika ngome zake,” asema Fred Musau, aliyekuwa mgombeaji wa kiti cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA) 2022.
Hata hivyo, Bw Sonko anasisitiza kuwa anachofanya ni kutumia haki yake ya kikatiba. Kulingana naye, kuanzisha chama cha kisiasa si mapinduzi wala hujuma, bali ni hatua anayofuata katika safari yake ndefu ya kisiasa.
“Ni haki yangu ya kikatiba na kidemokrasia kuanzisha na kuwa na chama,” Sonko alisema.
“Ninaheshimu sana kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, na hili halihusiani na chama chake au ushawishi wake. Hata alinipigia simu kunipongeza.”
Anakanusha madai yanayoongezeka hasa kutoka ndani ya Wiper, kwamba chama chake ni mradi wa Serikali ulioanzishwa na Rais William Ruto kuharibu muungano wa upinzani unaoongozwa na Rigathi Gachagua na Kalonzo.
“Chama changu si mwanachama wa Muungano wa Upinzani, wala si mradi wa Ruto,” anasisitiza.
“Kama ningekuwa mradi, kwa nini Serikali ilifunga akaunti zangu na kunizuia kutumia fedha zangu? Nia yangu ni kuwa Rais siku moja.”
Lakini licha ya ujasiri wake hadharani, kuna chuki dhidi ya kile anachokiita kesi za kisheria zinazotumika kisiasa.
“Sheria imetumika kwa ubaguzi dhidi yangu. Mahakama zimetumika kujaribu kudhoofisha kazi yangu ya kisiasa. Tutapigana hadi haki itendeke. Ni kosa kutangaza kifo changu kisiasa,” alisema.
Mnamo Jumanne, Sonko alipokea cheti cha usajili wa chama na akatangaza nia yake ya kurejea katika siasa za jiji na nchi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
“Tunakaribisha kila mtu kutoka kizazi cha Gen Z hadi wazee, kutoka asili zote za kisiasa na yeyote anayelenga kubadilisha nchi yetu. Tushirikiane na tufanye kazi pamoja. Tutajikita katika kuwahudumia Wakenya,” alisema Sonko.