Habari

Stevo arudi Kenya baada ya kuponyoka kitanzi Saudi Arabia

Na DANIEL OGETA July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BAADA ya miaka 14 katika gereza la Saudi Arabia kiwemo kadhaa akisubiri kunyongwa, hatimaye Stephen Munyakho, anayejulikana sana kama Stevo, amerudi nyumbani Kenya.

Kurejea kwake mapema alfajiri Jumanne, kuliashiria mwisho wa safari ya mateso na mwanzo wa kuungana na familia iliyokuwa  imejaribu juu chini kuona kuwa anapata uhuru wake.

Akiwa na umri wa miaka 51, Munyakho alirejea katika maisha ambayo yalikuwa yameendelea bila yeye kuwepo.

Aliondoka umri wake ukielekea mwisho wa miaka ya thelathini, na sasa amerudi kupata watoto wake wamekua, maswali mengi ambayo hayajajibiwa, na jamii iliyoshikilia tumaini licha ya kila hali.

Siku yake ya kwanza nyumbani ilitumika kujulishwa mambo aliyokosa, kama watoto wake watatu waliokomaa akiwa gerezani na juhudi za familia na marafiki waliopigania uhuru wake bila kukoma.

Ndege aliyosafiria kutoka Jeddah ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta saa sita na dakika 50 usiku.

“Uwepo wangu hapa leo ni muujiza wa kweli. Ni furaha kubwa kurudi nyumbani. Lakini tafadhali nipeni muda kidogo nipumzike na nijipange kabla sijaongea zaidi,” alisema.

Nje ya jumba la wageni mashuhuri katika uwanja wa ndege, umati mdogo lakini uliojawa furaha wa jamaa, marafiki na wafuasi ulikuwa umekusanyika, wengi wao wakiwa wamevaa mashati tao maalum na kushika mabango yaliyoandikwa ujumbe wa matumaini ulioendelezwa kwa muda mrefu: #BringBackStevo.

Akiwa amevalia shati la rangi ya buluu hafifu na suruali ya kaki, Stevo alitokea akiwa ameandamana na wazazi wake — mama yake, mwanahabari na mhariri wa miaka mingi Dorothy Kweyu upande wa kushoto na baba yake Reuben Maero upande wa kulia.

Aliinua mkono kwa ishara ya kuwasalimu waliokuwa wakishangilia, lakini hisia zilimzidi haraka na machozi yakaanza kumtiririka mashavuni alipokaribishwa kwa wimbi la maombi, salamu na vilio vya furaha.

“Asante Yesu. Asante Allah, kwa zawadi hii ya maisha. Asante kwa kila mmoja,” alisema mama yake akiwa amejawa na hisia.