Habari

Tafadhali msisafiri mashambani, wakazi wa mijini waombwa

March 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

WAKAZI wa mijini wameshauriwa wasisafiri kuelekea mashambani wakati huu ambapo serikali inajitahidi kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya, alisema kwa kusafiri mashambani, wakazi hao wanajiweka wao pamoja na jamaa zao katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo.

Ushauri huo pia unazingatia kwamba, kuna wazee wengi wanaoishi mashambani, na wazee wametambuliwa kuwa katika hatari zaidi ya kupata madhara makubwa endapo wataambukizwa.

Bw Oparanya aliongeza kuwa njia bora ya kujikinga na virusi hivyo ni kuosha mikono kwa sabuni kila mara na kuepuka maeneo yaliyo na watu wengi.

“Kusafiri ni kujiweka katika tisho kubwa kwa sababu magari ya uchukuzi wa umma yametambuliwa kuwa hatari katika kueneza virusi hivi. Kaa ulipo na uzingatie kunawa mikono kwa sabuni na kutohudhuria mikutano ya watu wengi,” akasema.

Kwa upande mwingine, Gavana wa Machakos Alfred Mutua alisema wazee wanahitaji kulindwa kikamilifu.

“Tunajua virusi hivi vinaathiri zaidi watu wazee walio na umri wa miaka 70 na 80. Hawa ndio wamekufa kwa wingi katika mataifa ya ng’ambo. Kwa hivyo kuna haja ya kuwakinga wazee wetu,” akasema Dkt Mutua.

Wawili hao walisema hayo baada ya kuripotiwa kuwa wakazi wengi wa mijini hasa Nairobi wameanza kusafiri kwenda mashambani tangu kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilipotangazwa nchini Ijumaa wiki iliyopita.

Baadhi ya kampuni zimepunguza oparesheni na kuwataka wafanyakazi kuchukua likizo bila malipo.

Magavana hao pia walitoa wito wa kusaidiwa kwa vifaa vinavyohitajika kukabili maradhi hayo.

“Tunamuomba waziri wa afya kuchukulia suala hili kwa uzito na kuhakikisha nchi inapata vifaa vya kutosha kusaidia kuzuia virusi hivi,” alisema Bw Oparanya.

Magavana walisema kaunti zinazopakana na nchi majirani zinahitaji rasilmali zaidi ili kuzuia virusi hivyo kupenya mipakani.

Walilalamika kuwa kaunti zimepokea vifaa 2,805 pekee vya kujikinga licha ya kuahidiwa vifaa 305,000.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha kila kaunti itakuwa na vifaa vya kutosha.

“Kila kaunti ilipatiwa vifaa vitano vya kukagua na kuanzia leo, serikali itatoa vifaa zaidi kwa kaunti kulingana na mahitaji ya kila moja,” akasema Bw Kagwe.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Gavana wa Embu Martin Wambora alisema watu wanaoshukiwa kuwa na virusi hivyo katika kaunti wanalazimika kusubiri kwa muda mrefu kwa sababu vipimo vinafanyiwa Nairobi pekee.

“Hatuwezi kuwapima kwa sababu hii haijaruhusiwa. Tunapaswa kuwa na vituo vya kupima katika hospitali zote za kaunti,” alisema Bw Wambora.