Habari

Taharuki bloga na mkosoaji wa Rais Ruto akitekwa nyara Baringo

Na FLORAH KOECH July 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUTEKWA nyara kwa mkosoaji mkubwa wa serikali Vincent Kipsang, ambaye alijitangaza Mwenyekiti wa DCP Kaunti ya Baringo kumezua taharuki mjini Kabarnet.

Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni bloga anayefahamika kama ‘Zonko Classic’ kwa mujibu wa wenyeji, alidaiwa kutekwa nyara Jumapili jioni na watu wasiojulikana.

Alibebewa juu juu na kuwekwa kwenye subaru kisha wakaondoka naye na hadi leo bado hajulikani aliko.

Bw Kipsang ni mkosoaji mkubwa wa Rais William Ruto na ni kati ya wale ambao wamekuwa wakiendeleza kauli mbiu ya ‘muhula moja’.

Kauli hiyo imekuwa ikishabikiwa Baringo na maeneo jirani.

Kwa mujibu wa mashahidi, alitekwa nyara na watu waliokuwa kwenye Subaru mbili na gari aina ya Toyota Land Cruiser.

Walimchukua kutoka kwa duka lake kisha wakaenda naye eneo kusikojulikana.

Wanafamilia wake, wanaharakati na baadhi ya wanajamii sasa wanadai alitekwa nyara kutokana na sababu za kisiasa kwa sababu ya kukosoa utawala wa Kenya Kwanza mara kwa mara.

Walioshuhudia akitekwa nyara walisema kuwa waliomchukua walisema wao ni maafisa kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI).

Mkewe Kipsang’ Angela Chesang alisema tukio lilifanyika haraka na watoto waliokuwa wakicheza nje ya duka wakagundua na kupiga nduru.

“Nilitoka nje ya nyumba ambayo ipo karibu na duka na kupata mlango ukiwa umefunguliwa. Gari lilikuwa limeondoka na mumewe wangu hakuwa popote,” akasema Bi Chesang’.

Baada ya muda alipokea simu kutoka kwa mumewe aliyemtaka apeleke kitambulisho chake kituo cha polisi cha Kabarnet.

Baada ya kuwasili aliambia ampokeze afisa mmoja wa polisi kitambulisho chake kisha amsubiri katika kituo cha polisi cha Muthaiga, Nairobi.

Alipowasili Nairobi, alijaribu kumfikia lakini simu yake ilikuwa imezimwa.

“Kama alitenda kosa naomba serikali ihakikishe hajaumizwa. Wampeleke kortini na ashtakiwe kwa sababu yeye ndiye tegemeo kwa famalia yetu na bado ni mdogo, naomba tu apatikane salama,” akasema.

Kamanda wa Polisi wa Baringo Julius Kiragu aliambia Taifa Leo kuwa hafahamu chochote kuhusu kisa hicho na Bw Sang hakuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabarnet.

“Sina habari na hakuna ripoti kuwa aliletwa na kuzuiliwa hapa. Kama alichukuliwa, fuatilia na DCI,” akasema Bw Kiragu.

Afisa wa Uchunguzi wa Uhalifu (CCIO) Kaunti ya Baringo pia alizungumza kwa tahadhari akisema huenda Bw Kipsang’ anazuiliwa na maafisa wa DCI Nairobi.

“Sina habari lakini mkewe anasema alipelekwa Kabarnet kisha Muthaiga Nairobi. Hapo alikamatwa wala si kutekwa nyara,” akasema Bw Gichimi.