Taharuki majangili wakimuua padri kwa kumpiga risasi
KISA ambapo kasisi wa kanisa la Kikatoliki alipigwa risasi na kuuawa katika kijiji cha Kabartile, eneo la Tot, Bonde la Kerio kimezua taharuki miongoni mwa wakazi eneo hilo.
Kulingana na polisi, Kasisi Allois Cheruiyot Bett, wa Kanisa la St Mathias Mulumba, Parokia ya Tot, aliandamwa na kuuawa na washambulizi waliojihami kwa bunduki.
Kisa hicho kilitokea kasisi alipokuwa akielekea makao makuu ya parokia baada ya kukamilisha ibada yake ya kila siku kijijini humo.Kamanda wa Polisi, Bonde la Kerio, Zablon Okoyo alithibitisha tukio hilo akisema OCS wa Kituo cha Polisi Tot alizuru eneo la tukio na kutwaa mwili uliopelekwa mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Moi (MTRH).“Kasisi alikuwa kwenye shughuli zake za kila siku kijijini Kabartile, eneo la Mokoro, na alikuwa anaelekea Tot alipofuatwa na washambulizi waliojihami waliompiga risasi kabla ya kutorokea vichakani. Kasisi alikufa papo hapo,” alisema Bw Okoyo.“Polisi sasa wanachunguza kuhakikisha washambulizi wamekamatwa na kufikishwa kortini. Bado hatujabainisha kiini cha mauaji,” alisema.Kulingana na taarifa aliyotoa msemaji wa polisi, Muchiri Nyaga, Alhamisi, washukiwa wanaohusishwa na mauaji hayo wamekamatwa na kurushwa korokoroni.“Uchunguzi wa mwanzo unafichua kwamba kisa hicho hakihusiani kwa vyovyote na wizi wa mifugo wala ujangili. Tunasihi jamii eneo hili kudumisha utulivu na kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu na kushirikiana na polisi,” alisema Bw Nyaga.Japo polisi wamesema hayahusiani na ujangili, mauaji ya kasisi yamezua hofu miongoni mwa wakazi wanaohusisha kifo chake na mashambulizi yanayolenga mabalozi wa amani na wasio wenyeji wanaokisiwa kuwa “wapelelezi.”Bonde la Kerio lilifurahia utulivu kwa karibu miezi tisa baada ya serikali kuimarisha usalama ikiwemo kutuma vikosi vya usalama katika maeneo yaliyosheheni majangili na kuweka kambi za usalama sehemu zinazoaminika kuwa mikondo yao ya kutorokea.Hata hivyo, mashambulizi mapya yalizuka mwanzoni mwa mwaka huu na kuwaua watu zaidi ya 22 katika kaunti za Baringo na Elgeyo Marakwet huku wengine kadhaa wakiuguza majeraha ya bunduki.Majangili wamebadilisha mbinu ambapo wanavamia ghafla na kuua kabla ya kutoweka bila kuiba wanyama ili kuwakwepa maafisa wa usalama ambao wamekita kambi eneo hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja ili kurejesha utulivu.Mabalozi watatu wa amani waliuawa Januari iliyopita kwa kupigwa risasi na wavamizi waliojihami huku watu wengine wawili wakiuawa wiki iliyopita na kuzua taharuki miongoni mwa wakazi.Wahasiriwa wanaojumuisha wazee wawili na mwalimu wa shule ya msingi kutoka Chesongoch, Marakwet Mashariki, walikuwa kwenye oparesheni ya kupokea mbuzi wanne kutoka kwa wanajamii wenzao Wapokot, walipouawa na majangili kwenye barabara ya Murkutwo-Kerio.