Taharuki yatanda kwa Gavana Natembeya maafisa wa EACC, DCI wakitaka kumkamata
TAHARUKI imetanda katika makazi ya Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya katika mtaa wa Milimani, Kitale baada kikosi cha maafisa wa kukabiliana na ufisadi EACC na DCI kuvamia nyumba yake Jumatatu asubuhi.
Maafisa hao waliwasili katika boma hilo saa moja asubuhi wakiwa wamesindikizwa na polisi wa kupambana na ghasia.
Lakini wakazi waliovutiwa na uwepo mkubwa wa polisi walizingira na kuingia ndani kupinga kupekuliwa kwa nyumba ya Gavana Natembeya.
Vijana walitoboa magurudumu ya magari matano waliyokuja nayo maafisa hao.
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa na madiwani kadhaa wamo katika boma hilo. Bw Wamalwa anasema Gavana hakuwa nyumbani wakati wa uvamizi huo.
“Nimeongea na Gavana na yuko salama mahala fulani Nairobi. Huu ni unyanyasaji mkubwa zaidi kufanywa na serikali,” akasema.
Baadhi ya wanahabari waliokuwa wanafuatilia matukio walipigwa na vijana wenye ghadhabu.
Habari zaidi ni kadiri zinavyotufikia…