Taharuki yatanda Outering Road, Kariobangi wahuni wakihangaisha wahudumu wa matatu
TAHARUKI imetanda katika vituo vya matatu vya Harmony 25 na 26 katika mtaa wa Kariobangi kando ya Barabara ya Outering, Nairobi, ambako makabiliano kati ya wahudumu yamechangia wengi kujeruhiwa na magari kuharibiwa.
Fujo zilianza wiki jana pale genge lililoaminika kukodiwa, lilivamia kituo hicho kwa kuwarushia wahudumu mawe vijiti na chupa.
Wahudumu wa matatu nao walikabiliana nao vikali katika mapambano yaliyodumu kwa saa siku kadhaa.
Kufikia mapema wiki hii, matatu sita yalikuwa yameharibiwa katika vurugu hizo huku vioo vikitapakaa katika barabara ya Outering.
“Walikuwa wengi zaidi. Mmoja alijaribu kunipiga kwa chupa. Nilipokuwa nikizuia chupa, mwingine alinikata kichwa kwa upanga,” akasema Jonathan, mhudumu wa matatu, huku akituonyesha jeraha kichwani mwake.
Kando yake alisimama George Ang’wena, ambaye pia bado anauguza majeraha.
Wakazi wa eneo hilo wanasema huenda fujo hizo zimechochewa kisiasa.
Baadhi ya wahudumu walisema wavamizi hao waliletwa na mwanasiasa fulani.
“Ghasia hizi hazijasababishwa na mvutano kuhusu vituo vya matatu. Zimechochewa na mwanasiasa,” akasema mwenyekiti wa kituo hicho cha matatu Billy Ojura.
“Tangu diwani wetu Joel Munuve alipokufa Aprili mwaka huu tumeachwa bila mtetezi.
Mvutano kuhusu kituo hicho cha matatu umekuwepo kwa miaka mingi.
Kulingana na Joseph Majo, ambaye ni dereva wa matatu moja ya chama cha ushirika cha Manimo Sacco, alisema taharuki ilianza mnamo 2016 wakati matatu ya ruti 26 yalipoanza kuhudumu kutoka eneo la mzunguko.
Baadaye kuundwa upya kwa mzunguko wa barabara ya Outering kuliwagawanya wahudumu hao kuwili; Ruti 25 na Ruti 26.
Lakini sasa kulingana na Bw Majo wahuni waliokodiwa kutoka Buruburu na Kariobangi South wanatumika kutwaa udhibiti wa kituo hicho cha matatu.
“Hawa watu hawana magari yao. Wao hutokea tu wakiwa na visu na chupa wakitaka kutwa kile ambacho tumeunda. Na wanalipwa kufanya hivyo. Kufikia sasa wameharibu magari 20. Hatuko salama hata nyakati za mchana—mashambulio yanafanyika asubuhi, adhuhuri na jioni,” akasema.
Wahudumu hao wanasema wamepiga ripoti kwa vituo kadhaa vya polisi kuhusu suala suala hilo, lakini hawajasaidia.
Isitoshe, wanasema, maafisa wa usalama wanaonekana kuwaunga mkono wavamizi hao.
TAFSIRI: CHARLES WASONGA